Hemed ataja fursa uchumi wa buluu, akaribisha wawekezajiHemed ataja fursa uchumi wa buluu, akaribisha wawekezaji

Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema Zanzibar ina fursa kubwa za uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu, ikiwamo ufugaji wa viumbe maji, usindikaji wa mazao ya baharini, bioteknolojia ya baharini na utalii wa mazingira.

Mbali na sekta hizo, amesema pia kuna nafasi za uwekezaji katika usafirishaji wa baharini, kaboni ya buluu, suluhisho za uchumi mzunguko pamoja na teknolojia za kidijitali za baharini.

Hemed amesema hayo leo Mei 25, 2026 wakati akifungua warsha ya 29 ya watunga sera, watafiti na viongozi wa sekta binafsi kutoka nchi mbalimbali za Afrika iliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa) kwa kushirikiana na Wizara ya Uchumi wa Buluu, Tume ya Taifa ya Mipango na CRDB Bank.

“Hivyo tunawakaribisha wawekezaji walio tayari kuwekeza katika sekta hii kwa sababu Zanzibar tayari imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji,” amesema Hemed.

Amesema vijana wengi wameanza kujikita katika biashara bunifu zinazohusisha bidhaa za mwani, ufugaji wa viumbe maji, utalii wa mazingira, teknolojia ya baharini, kazi za mikono endelevu na huduma za kidijitali za baharini.

Hemed amesema hali hiyo inaonesha kuwa uchumi wa buluu hauishii kwenye shughuli za uvuvi na usafirishaji wa baharini pekee, bali pia ni eneo la ubunifu, teknolojia na ujasiriamali.

Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika mafunzo ya baharini, matumizi ya droni, ufugaji wa kisasa wa viumbe maji na uundaji wa mifumo ya bahari ili kuwajengea vijana ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la sasa na la baadaye.

“Uchumi wa buluu ni zaidi ya sekta ya kiuchumi, ni safari ya pamoja ya taifa inayohitaji uwajibikaji, ubunifu, tafiti imara pamoja na ushirikiano wa kikanda na kimataifa,” amesema.

Akizungumza katika warsha hiyo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Tanzania Bara, Denis Rondo amesema mkutano huo unakuja katika kipindi muhimu cha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo kwa kiasi kikubwa inategemea ushiriki wa sekta binafsi.

“Moja ya rasilimali kubwa tulizonazo ni maziwa na bahari. Nchi imebarikiwa kuwa na eneo kubwa la maji hivyo ni lazima litumike ipasavyo ili kusaidia utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kupunguza umasikini,” amesema Rondo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari amesema dhana ya uchumi wa buluu inalenga kuleta mapinduzi ya kiuchumi kupitia matumizi sahihi ya rasilimali za bahari kwa ushirikiano wa kikanda.

Amesema changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa hewa ukaa na kupanda kwa kina cha bahari ni miongoni mwa masuala yanayohitaji kupewa kipaumbele katika tafiti na utungaji wa sera.

“Tunaangalia namna tafiti zinavyoweza kusaidia kubaini maeneo ya vipaumbele ili kuhakikisha uchumi wa buluu unakuwa endelevu na jumuishi,” amesema Dk Mmari.

Naye Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Masoud Ali Mohamed amesema uwekezaji katika tafiti una mchango mkubwa katika kukuza sekta hiyo na kwamba wizara yake imeendelea kushirikiana na Repoa kuimarisha mazingira ya uchumi wa buluu kupitia tafiti mbalimbali.

Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank, Neema Mori amesema benki hiyo imekuwa mdau mkubwa wa uwezeshaji wa kifedha katika sekta ya uchumi wa buluu ambapo zaidi ya wanufaika 50,000 tayari wamefikiwa.

“Tunashirikiana kuhakikisha tunawezesha mnyororo wa thamani pamoja na miundombinu inayohitajika katika miradi ya uchumi wa buluu,” amesema Profesa Mori.

Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Blandina Kilama amesema tafiti ni msingi muhimu wa mipango ya maendeleo.

“Huwezi kupanga bila kutumia tafiti. Lazima ujue hali halisi na maeneo ya kuwekeza nguvu ili uchumi wa buluu uweze kuleta matokeo chanya,” amesema Kilama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *