Chalamila amkingia kifua Mafwele, Jeshi la PolisiChalamila amkingia kifua Mafwele, Jeshi la Polisi

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka Watanzania kuacha tabia ya kutoa hitimisho la haraka kuhusu matukio ya uhalifu yanayotokea nchini kabla vyombo vya dola kukamilisha uchunguzi wake.

Akizungumza leo Mei 25,2026 jijini Dar es Salaam kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu yaliyotokea hivi karibuni, Chalamila amesema tabia ya baadhi ya watu kuanza kuelekeza lawama au kutoa tafsiri za kisiasa mapema inakwamisha uchunguzi na inaweza kupotosha jamii.

Kauli hiyo imekuja huku kukiwa na mjadala mkubwa mitandaoni na kwenye majukwaa mbalimbali kufuatia taarifa za kuuawa kwa mfanyabiashara raia wa China, Bhaozang Ge pamoja na kudaiwa kutekwa kwa msaidizi wa Tundu Lissu, David Djumbe.

Mfanyabiashara na mmiliki wa kiwanda cha XIL LI, Bhaozang Ge (50), aliuawa na watu wanaodaiwa ni walinzi binafsi wa kiwanda chake kilichopo Mabibo, jijini Dar es Salaam saa 8 usiku wa kuamkia Jumamosi ya Mei 16, 2026.

Pia, David Djumbe ambaye ni Msaidizi wa Tundu alidaiwa kutekwa kabla ya kufanikiwa kutoroka Mei 20 mwaka huu akiwa anaelekea nyumbani kwake Bunju akiwa na rafiki yake Allan Macha wakiwa kwenye gari.

Chalamila amesema mara nyingi matukio ya uhalifu yanapopewa tafsiri za kisiasa kabla ushahidi haujakamilika, huathiri kazi ya uchunguzi inayofanywa na Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama.

“Jambo lolote linapotokea katika taifa, hasa la mauaji, wizi au uhalifu mwingine, wahalifu hawachagui itikadi. Anaweza kumdhuru mtu yeyote bila kujali chama chake cha siasa,” amesema Chalamila.

Amesema kitendo cha baadhi ya wananchi kufikia hatua ya kuwataja watu wanaodhani wanahusika kabla ya uchunguzi kukamilika inaweza kuwafanya hata maofisa kushindwa kutoa taarifa kwa wakati kutokana na mazingira ya lawama na mashinikizo ya kijamii.

“Mtu anaweza kusema nimeona kwenye mitandao kwamba aliyefanya hivyo ni Mafwele (Faustin, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Tanzania). Sasa huyo huyo Mafwele ndiye anayesimamia uchunguzi kwenye dawati. Hata kama ana majibu sahihi, anawezaje kuja kutoa kwa Watanzania wakati baadhi yetu tayari tumeshakuwa na majawabu kabla uchunguzi haujakamilika?” alihoji.

“Mkishakuwa na majawabu tayari kuhusu tukio fulani, mnakuwa mnazuia hata wale wanaofanya uchunguzi kuendelea vizuri. Wakati mwingine ushahidi bado unakusanywa lakini tayari watu wamekwisha kutoa hukumu,” amesema.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, mazingira ya matukio ya kihalifu hutofautiana, hivyo kasi ya upatikanaji wa majibu pia hutegemea ushahidi uliopo, teknolojia inayotumika, namna tukio lilivyofanyika pamoja na muda lilipotokea.

Amesema si matukio yote yanaweza kutatuliwa kwa muda unaofanana, jambo ambalo wananchi wanapaswa kulielewa.

“Uchunguzi ni jambo la ushahidi, ni jambo la teknolojia na mazingira ya tukio lenyewe. Huwezi kulinganisha matukio yote,” amesema.

Chalamila ametolea mfano wa tukio la kuuawa kwa mfanyabiashara raia wa China, akisema kama marehemu angekuwa mwanasiasa anayejulikana waziwazi kwa chama fulani, kuna uwezekano watu wangeanza kutoa tafsiri za kisiasa mapema.

“Labda angekuwa anafahamika kuwa ni mwanachama wa chama fulani, watu wangesema ameuliwa kwa sababu ya itikadi yake. Lakini kwa kuwa hilo halipo, uchunguzi wake unaendelea katika mazingira ya kawaida,” amesema.

Aliwataka wananchi kuendelea kuwa na imani na vyombo vya usalama huku akisisitiza kuwa hali ya usalama katika Mkoa wa Dar es Salaam ipo shwari.

“Kwanza nitoe wasiwasi kwa wananchi wote kwamba hali ya usalama katika Mkoa wa Dar es Salaam ni nzuri sana. Pia niwasihi wawekezaji na wananchi wanaomiliki maeneo makubwa ya biashara hakikisheni mnatumia walinzi kutoka kampuni rasmi zilizosajiliwa na Serikali badala ya kuajiri watu binafsi,” amesema.

Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia walinzi wasiokuwa na usajili wala mikataba rasmi kwa sababu ya kutaka kupunguza gharama, jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wao na mali zao.

“Ukikuta unalindwa na mtu yeyote, hakikisha anatoka kwenye kampuni iliyosajiliwa na inayotambulika. Watu wengi wanapenda kutumia ‘cheap labour’ kwa sababu ni rahisi lakini wanataka walindwe mali za mabilioni,” amesema.

Kauli hiyo imekuja baada ya taarifa kueleza kuwa baadhi ya watu waliokuwa wakifanya kazi ya ulinzi katika eneo la mfanyabiashara raia wa China aliyeuwawa walitoweka baada ya tukio hilo kutokea.

Chalamila amesema Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam inalichukulia kwa uzito tukio hilo pamoja na matukio mengine ya uhalifu yanayojitokeza, huku akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi.

Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha wawekezaji wanakuwa salama na wanaendelea kuwekeza nchini bila hofu.

“Tunalaani sana matukio haya. Wawekezaji wasiogope kuendelea kuja kuwekeza nchini kwetu. Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha matukio kama haya yanakomeshwa,” amesema.

Pia, amezungumzia tukio la kutoweka kwa mtu anayetajwa kuwa msaidizi wa mfanyabiashara Jumbe, akisema Serikali ya Mkoa inalilaani kama inavyolaani matukio yote ya kihalifu bila kujali tofauti za kisiasa, kidini au kijamii.

“Masuala ya uhai na usalama hayana chama. Awe mwanachama wa Chama cha Mapinduzi, Chadema au CUF, tukio la kihalifu tunalilaani kwa nguvu zote,” amesema.

Katika msisitizo wake wa mwisho, Chalamila amesema sheria itachukua mkondo wake dhidi ya yeyote atakayebainika kuvunja sheria bila kujali nafasi yake katika jamii.

“Usije ukadhani kwamba ukiwa kwenye chama fulani cha siasa au taasisi ya dini utaogopwa. Sheria itafanya kazi sawa kwa kila mtu,” amesema.

Chalamila pia amerejea tukio marehemu James Temba akielezea namna baadhi ya watu walivyokuwa wakitoa matamko ya haraka kabla uchunguzi haujakamilika kama mfano wa changamoto inayozikabili mamlaka za uchunguzi nchini.

“Mliona namna lile tukio la bwana Temba lilivyoanza, huyu akatoa barua ya kusikitishwa, mwingine akatoa taarifa ya kusikitishwa, mpaka ikaanza kuonekana kama tayari kuna upande fulani umehusika,” amesema.

Chalamila amesema matukio mengi ya kihalifu yanahitaji muda, ushahidi na uchambuzi wa kitaalamu kabla ya vyombo vya dola kutoa majibu rasmi, hivyo wananchi wanapaswa kuepuka kutoa hitimisho la haraka ambalo linaweza kupotosha uchunguzi au jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *