
Marekani imemuwekea tena vikwazo Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu kwa sababu tu ya kufichua mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Wizara ya Fedha ya Marekani iliandika kwenye tovuti yake jana Jumatano kwamba imemuwekea tena vikwazo vya kifedha Francesca Albanese. Taarifa hiyo ya Wizara ya Fedha ya Marekani imetolewa baada ya Jaji wa Shirikisho wa Marekani, Richard Leon, kusimamisha vikwazo vya serikali ya Washington dhidi ya Albanese katikati ya mwezi Mei.
Albanese, ambaye ni Muitaliano, amekuwa mstari wa mbele kuukosoa utawala katili wa Israel kwa mauaji ya kimbari ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 2023, na pia kwa mauaji mengine ya utawala huo katika Ukingo wa Magharibi. Amekuwa akikosoa vikali ukatili wa Israel dhidi ya Wapalestina katika nafasi yake kama Ripota Huru Maalumu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.
Francesca Albanese ameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kufanya uchunguzi dhidi ya maafisa wa Israel na Marekani, na kuwafungulia mashtaka watu waliohusika na mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Gaza.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imemshutumu Albanese kwa kufuatilia uchunguzi “usio halali na usio na msingi” kuhusu vitendo vya mauaji ya kimbari vya Israel huko Gaza na mienendo ya kijeshi wa Marekani.
Vikwazo hivyo vinamzuia Albanese kuingia Marekani na kufanya miamala ya kibenki.
Jaji Leon alisema katika uamuzi wake mapema mwezi huu kwamba vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Albanese vilikiuka haki zake. Alieleza kuwa vikwazo alivyowekewa na serikali ya Marekani vilitokana na wito wake wa kuwajibika kwa mahakama ya ICC.
“Albanese hajafanya chochote zaidi ya kuzungumza,” aliandika Jaji Leon.
