IRIB yalaani mauaji ya Israel dhidi ya mwandishi habari wa al-Alam kusini mwa LebanonIRIB yalaani mauaji ya Israel dhidi ya mwandishi habari wa al-Alam kusini mwa Lebanon

Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB), Peyman Jebelli, na Kitengo cha Matangazo ya Ng’ambo cha IRIB wamelaani vikali mauaji ya Hesam Zidan, mwandishi wa habari wa zamani wa chaneli ya televisheni ya al-Alam ya Iran nchini Syria, ambaye ameuawa katika shambulio la Israel kusini mwa Lebanon.

Katika ujumbe uliotolewa jana Alhamisi, Jebelli alisema kwamba “kuuawa shahidi Zidan, shujaa wa uwanja wa habari na mwandishi habari aliyeazimia wa vyombo vya habari vya Kambi ya Muqawama katika shambulizi la kihalifu la Wazayuni dhidi ya Sidon, kumefichua tena sura halisi na hulka mbaya ya utawala ghasibu wa Israel.”

Ameongeza kuwa Israel imeazimia kuwalenga waandishi wa habari wanaofichua uhalifu unaofanywa na vikosi vyake kote katika eneo la Asia Magharibi.

“Msisitizo wa utawala wa Kizayuni wa kuwaua waandishi wa habari ni ishara ya hofu kubwa ya utawala huo, ambao ni kieleleo cha giza, ya kufichuliwa nuru ya ukweli,” amesema Peyman Jebelli.

Ameongeza kusema kwamba “utawala huo muovu unajua vyema kwamba mauaji ya Zidan na vinara wengine wa heshima na hadhi ya juu ya binadamu sio mwisho, bali mwanzo wa ushindi wa muqawama.”

Jebelli pia ametoa rambirambi kwa familia ya Hesam Zidan, jamii ya vyombo vya habari vya kikanda, na “waandishi wote wa habari wanaopigania haki na ukweli.”

Katika taarifa tofauti, Kitengo cha Matangazo ya Ng’ambo cha IRIB (IRIB World Service) imesema kwamba “kuuawa shahidi mwenzatu mpendwa kufuatia shambulio la anga la utawala wa Israel katika mji wa Sidon kusini mwa Lebanon kumefichua tena sura halisi ya utawala huo wa kihalifu.”

“Alikuwa miongoni mwa waandishi wa habari waliotekeleza dhamira yao ya kitaaluma si kutoka nyuma ya dawati la habari, bali kutoka mstari wa mbele na katikati ya uwanja wa mapambano,” imesema taarifa hiyo.

“Sisi, IRIB World Service, huku tukilaani uhalifu huu wa wazi, tunatuma rambirambi zetu kwa familia ya shahidi Zidan, wafanyakazi wenzake wa vyombo vya habari, watu wa Lebanon na Syria, na watu wote huru duniani,” imesema taarifa hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *