Unguja. Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi imeainisha vipaumbele vinne, kuimarisha uvuvi wa bahari kuu, kununua meli kubwa za uvuvi na ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki.

Pia, imepanga kuanzisha eneo huru la uwekezaji wa Uchumi wa Buluu Fungurefu na kuimarisha sekta ya mafuta na gesi asilia, kwa kufanya utafiti wa utafutaji wa rasilimali hiyo kwa njia ya mtetemo ya 2D na 3D pamoja na kujenga Kituo cha kudumu cha kuhifadhia taarifa za mafuta na gesi asilia.

Hayo yamebainishwa leo Mei 30, 2026 na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Masoud Ali Mohamed wakati akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo mwaka 2026/27 katika mkutano wa 11 wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Unguja Zanzibar.

Katika hotuba yake Waziri Masoud ameomba baraza kuidhinisha Sh209 bilioni ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele hivyo.

“Katika kuimarisha uvuvi wa bahari kuu serikali inakamilisha ununuzi wa meli kubwa za bahari kuu leongo ni kuhakikisha tunafikia maji marefu na kupata samaki wengi zaidi,” amesema.

Pia, Wizara imepanga kuendeleza uvuvi mdogomdogo kwa kufanya ujenzi wa madiko (mialo) na masoko ya kisasa ya samaki, kuanzisha maabara ya kisasa kwa ajili ya kuthibitisha mazao ya baharini katika soko la ndani na la nje pamoja na kuimarisha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.

Kwa upande wa zao la mwani, amesema litapewa hadhi zaidi kwa kujenga viwanda vidogovidogo na vikubwa vya kibiashara ili kusarifu zao hilo na kuongeza thamani pamoja na kuendelea kuwawezesha wakulima wa mwani kwa kuwapatia pembejeo na elimu iliyo bora ili kuongeza uzalishaji.

Kuimarisha sekta ya mafuta na gesi asilia kwa kufanya utafiti wa utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa njia ya mtetemo ya 2D na 3D pamoja na kujenga Kituo cha Kudumu cha kuhifadhia Taarifa za Mafuta na Gesi Asilia (NDR).

Maoni ya Kamati

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Uwekezaji, Makame Mohamed Sufiani amesema kamati inaishauri Serikali kuwekeza kwa ajili ya uendeshaji wa utafiti kuhusu mahitaji ya uvuvi.

Amesema kamati imebaini kuwa utafiti katika eneo hilo linahitaji bajeti kubwa katika utekelezaji wake.

“Kamati inaishauri Wizara kuwa na mipango endelevu ya kuandaa miundo mbinu ya kuwafikia samaki kwani kamati imebaini kuwa miundo mbinu iliyopo haikidhi haja katika soko la uchumi wa buluu,” amesema.

Kadhalika, kamati inaishauri Wizara kufanya mabadiliko ya sheria ya uvuvi itakayoanzishwa itakayozikabili changamoto zilizopo katika maendeleo ya uvuvi.

Katika kuhakikisha sekta ya mafuta na gesi asilia inafanikiwa Zanzibar, kamati imesema ipo haja ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa rasilimali fedha za ufuatiliaji, wataalamu katika kada hiyo.

Michango ya wawakilishi

Akichangia bajeti hiyo Mwakilishi wa Mkwajuni Sulubu Kidongo Amour (CCM) amesema inatakiwa kutunza bahari kwani inamuhimu zaidi.

Amesema boti nyingi zilizokopeshwa kwa wavuvi zinafanya kazi ya kupeleka watalii visiwani badala ya malengo yaliyokusudiwa kuendesha uvuvi.

Mwakilishi nafasi za Wanawake, Moza Mohamed Khamis (ACT Wazalendo) amesema iwapo uchumi wa buluu ukitumika vizuri utasadia kuondokana na tatizo la ajira huku akitaka bahari ilindwe ili kuongeza upatikanaji wa rasilimali zake.

Mwakilishi wa Gando, Said Ali Mbarouk amesema uchumi wa taifa unategemea zaidi wizara hiyo hivyo wanatakiwa kujitathmini katika masuala ya sera.

Hata hivyo, amesema kiwango cha fedha kinachotengwa na kupatikana kwa wizara hiyo hakioneshi uhalisia na mataakwa halisi.

“Katika bajeti ya mwaka 2025/26 ziliztengwa Sh174 bilioni katika wizara hii lakini mpaka Machi zimepatikana Sh20 bilioni sawa na asilimia 25 tu, kwakweli hapa utaona namna gani bado kuna shida.

Amesema, “katika baadhi ya mambo tuone umuhimu wake eneo kama la miradi ya maeneleo huwezi kutengewa asilimia 16 kisha utegemee maendeleo… hayawezi kuja kama mvua,” amesema

Naye mwakilishi naafsi za wanawake, Fatma Ramadhan Mandoba amesema lazima mkakati uwekwe zaiid katika kujenga viwanda ambavyo vitapunguza changamoto ya ajira na kuchukua sehemu kubwa ya vijana.

Amesema licha ya kuelezwa kwamba uzalishaji wa samaki umeongezeka kwa asilimia moja kutoka tani 74 mwaka 2024 hadi tani 79 mwaka 2025, lakini bado kuna uingizaji mkubwa wa samaki kutoka je ya Zanzibar hivyo akaitaka wizara kuliangalia jambo hilo kwa umuhimu wake.

“Katika bajeti hii hatujaona kwa namana gani imewahusisha wanawake, sisi sote mashahidi wanwake wana mchango mkubwa kwasasa, kwahiyo ipo haja kuhakiksha kundi hili linazingatiwa ili kuwasaidia katika shughuli zao za uzalishaji,” amesema

Naye Mwakilishi wa Pandani, Omar Fakih Hamad (ACT Wazalendo) amesema baraza limekuwa likipitisha bajeti kubwa za uchimbaji na utafutaji wa mafuta na gesi asilia lakini hawaoni matokeo.

“Katika bajeti yam waka jana tulihidhinisha Sh9 bilioni za utafiti lakini hatujaelezwa zimefanya nini na leo tunaomba bajeti ya Sh35 bilioni kwajili ya utafiti huohuo, hizi fedha zinafanya kazi gani,” amehoji

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *