Dodoma. Watu saba wamefariki dunia na wengine 17 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha basi dogo la abiria aina ya Coaster na lori katika eneo la Mlima Senkenke, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Ajali hiyo ilitokea Juni 2, 2026 asubuhi wakati Coaster lililokuwa likisafiri kutoka Singida kwenda Tabora lilipogongana na lori lililokuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza.
Kwa mujibu wa mashuhuda, lori hilo lilifeli breki na kugonga Coaster, hali iliyosababisha basi hilo kutumbukia korongoni.
Magari yaliyopata ajali eneo la Sekenke na kusababisha vifo vya watu saba na majeruhi 17.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Dk Peter Janga, amesema hospitali hiyo ilipokea majeruhi 17 pamoja na miili sita ya waliofariki dunia, huku majeruhi mmoja akifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.
“Tulipokea majeruhi 17 na miili sita ya waliofariki. Mgonjwa mmoja alifariki akiwa hospitalini, hivyo kufanya idadi ya vifo kufikia saba,” amesema Dk Janga.
Amesema majeruhi waliobaki wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea kuimarika.
“Magari hayo yaligongana na kusababisha Coaster kutumbukia korongoni. Hali hiyo ilisababisha majeruhi wengi, wengi wao wakiwa wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao,” amesema.
Mmoja wa majeruhi akiwa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba.
Mmoja wa majeruhi, Emmanuel Sande, amesema alikuwa akisafiri kwa basi hilo kutoka Singida kwenda Igunga mkoani Tabora wakati ajali hiyo ilipotokea.
Amesema wakati ajali inatokea alikuwa amelala kutokana na uchovu wa safari na alishtuka baada ya kusikia kishindo.
“Nilikuwa nimelala usingizi. Niliposhtuka nikakuta tumepata ajali. Namshukuru Mungu, pamoja na majeraha tuliyoyapata, tumenusurika,” amesema Sande.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida kuzungumzia ajali hiyo hazikufanikiwa. Awali simu yake ilipokelewa na msaidizi wake aliyesema alikuwa kwenye kikao, lakini alipotafutwa baadaye simu yake haikupokelewa.
Endelea kufuatilia Mwananchi…