
Wanajeshi wa Nigeria wanaoendesha oparesheni kwa jina “Hadin Kai” wamewaangamiza magaidi wasiopungua 50, akiwemo kamanda mkuu wa tawi la ISWAP lililoungana na kundi la Boko Haram.
Magaidi hao 50 waliuawa jana Jumatano katika operesheni kali za kukabiliana na ugaidi kaskazini mashariki mwa Jimbo la Borno nchini Nigeria.
Msemaji wa Makao Makuu ya Ulinzi ya Jeshi la Nigeria, Samaila Mohammad Uba, ameeleza kuwa wamefanikiwa kuwauwa magaidi 50 na kamanda wao kufuatia shambulio la anga lililofanywa na jeshi karibu na Kirta na Ariba Ciki katika eneo la Ziwa Chad, ambapo makamanda kadhaa wa ISWAP wameripotiwa kuuawa.
Miongoni mwa waliouawa ni Khalifa Umar ambayo ametajwa na jeshi la Nigeria kuwa mwanachama wa chombo kikuu cha maamuzi cha kundi la ISWAP.
Mwezi Mei mwaka huu, wanajeshi wa kikosi cha Oparesheni “Hadin Kai” pia waliwaangamiza magaidi 50 wa ISWAP walipojaribu kushambulia kambi ya kijeshi huko Buni Gari, katika Jimbo la Yobe kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Mwezi uliopita, jeshi la Nigeria lilitangaza kuuawa Abu-Bilal al-Minuki kiongozi mwandamizi wa ISWAP.
Makundi ya ISWAP na Boko Haram yameendelea kuibua changamoto kubwa za kiusalama kaskazini mashariki mwa Nigeria licha ya jeshi la nchi hiyo kufanikiwa mara kadhaa kuwaangamiza magaidi wa kundi hilo.