Chanzo cha picha, US Central Command
Iran imeshambulia kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Ghuba kulipiza kisasi duru ya hivi karibuni ya mashambulizi ya Marekani, yaliyokuja baada ya Donald Trump kusema kwamba ataishambulia Iran “kwa nguvu kubwa”.
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema imekamilisha siku ya pili mfululizo ya mashambulizi ya “kujilinda”, yaliyofanyika usiku mmoja baada ya Trump kusema kwamba Tehran ilikuwa imechukua “muda mrefu sana kufikia makubaliano” ya kumaliza vita.
Kwa kujibu, Iran ilisema imeshambulia vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Bahrain na Kuwait, ambayo ni malengo yale yale yaliyolengwa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa na Iran siku iliyotangulia.
Kuongezeka huku kwa mashambulizi ya kulipizana kisasi katika siku za hivi karibuni kumefanya juhudi za makubaliano ya usitishaji kuwa dhaifu kati ya nchi hizo mbili.
Baada ya shambulio la hivi karibuni la Marekani, milipuko ilisikika katika miji ya kusini mwa Iran karibu na Mlango bahari wa Hormuz, ambapo vikosi vya Marekani pia vilishambulia mifumo ya ulinzi wa anga, rada na maeneo mengine katika duru ya awali ya mashambulizi.
Katika ongezeko hili jipya la mzozo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) pia lilisema limepiga meli mbili za kubeba mafuta zilizokuwa zikivuka Mlango wa Hormuz, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran, ingawa hakukuwa na uthibitisho wa haraka kutoka vyanzo huru.
Hii ilikuja baada ya vyombo vya habari vya serikali ya Iran kuripoti kwamba Mlango bahari wa Hormuz ulikuwa “umefungwa kabisa kwa aina zote za meli”. Hata hivyo, CENTCOM ilisema kwamba “meli za kibiashara zinaendelea kupita kuingia na kutoka katika Mlango wa Hormuz”.
Bei za mafuta zilipanda muda mfupi baada ya kutangazwa kufungwa kwa njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa baharini na baada ya taarifa za shambulio dhidi ya meli hizo kutolewa.
Unaweza kusoma;