HAT TRICK aliyofunga katika mechi iliyopita imempa nguvu na matumaini ya kuwania tuzo ya kiatu cha mfungaji bora straika wa Pamba Jiji, Methew Tegis, huku akichekelea kufikia rekodi aliyoiweka msimu uliopita akiahidi kuipita.

Tegis raia wa Kenya ni miongoni mwa wachezaji wawili waliofunga mabao matatu katika mchezo mmoja ‘Hatitriki’ akiungana na staa wa Singida Black Stars, Mossi Nduwumwe na kushirikiria rekodi hadi sasa.

Straika huyo alifanya hivyo wakati akiiongoza Pamba Jiji kuishushia kipigo cha mabao 4-0 Mtibwa Sugar na kufikisha mabao 11, akiachwa matatu na kinara Feisal Salum wa Azam FC mwenye 14.

Staa huyo anayecheza soka la kulipwa Tanzania kwa mara ya kwanza, msimu uliopita akiitumikia Shabana FC ya Ligi Kuu nchini Kenya, aliibuka mfungaji bora kikosini kwa mabao 11, katika mechi 15 alizocheza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Tegis alisema anafurahia kufikia rekodi aliyoiweka msimu uliopita na kwamba kwa sasa anajipanga upya kwa mechi tatu zilizobaki kwa ajili ya vita ya ufungaji bora.

Alisema anafahamu ugumu ulivyo dhidi ya wachezaji wengine akibainisha lengo lake ni kuacha historia na heshima Ligi Kuu Bara kwake binafsi na timu yake kuipa matokeo mazuri.

“Mpira ndiyo kazi yangu, zaidi ni kumtanguliza Mungu kuhakikisha ninachofanya nafanikiwa, ushindani ni mkubwa ila kwa mwendelezo wangu nashukuru, najipanga na mechi zilizobaki kuona nafikia lengo langu,” alisema Tegis.

Nyota huyo aliongeza Ligi Kuu Bara ni ngumu yenye ushindani ambayo imemfanya kujifunza na kutengeneza maisha yake kwenye medani za soka Afrika ili kuendeleza kipaji chake.

kocha wa Pamba Jiji, Francis Baraza alisema hafurahishwi sana na mshambuliaji huyo licha ya kufunga mabao hat-trick na anaamini ana nafasi kubwa zaidi ya kufanya vizuri kuliko alichoonyesha hadi sasa.

“Ni jambo zuri kwake kufunga mabao matatu na kama kocha lazima nifurahie hilo kwa sababu mshambuliaji kazi yake ni kufunga, lakini ukweli nilitegemea afike hatua hii mapema zaidi,” alisema Baraza.

“Mimi namjua Tegis ni mshambuliaji mzuri sana, hata nikisema kati ya washambuliaji bora waliopo Tanzania sitakuwa nimekosea. Tatizo kubwa limekuwa kujipa presha ndogo ya kutafuta rekodi na kuwa na njaa ya kufunga kila mechi,” alisema.

Pamba ambayo imecheza mechi tatu kumaliza msimu, itacheza dhidi ya Mbeya City, JKT Tanzania na Coastal Union, huku kwenye msimamo ikiwa nafasi ya saba, ikifikisha jumla ya pointi 36.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *