
Pennsylvania, Marekani. Ufaransa inaungana na Mexico, Marekani, Ujerumani na Argentina kufuzu mapema hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuichapa Iraq mabao 3-0 katika mechi ya Kundi I iliyopigwa Uwanja wa Philadelphia, Marekani.
Mechi hiyo ambayo ilisimama kwa zaidi ya saa moja na nusu kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na radi, ilikuwa ya ushindani wa aina yake.
Nahodha wa kikosi hicho, Kylian Mbappe alikuwa nyota wa mechi hiyo baada ya kufunga mabao mawili dakika ya 14 na 54 kabla ya Ousmane Dembélé kuongeza la tatu dakika ya 66 na kuifanya Les Bleus kushinda mechi zote mbili kwenye kundi hilo ikifikisha pointi sita kileleni mwa kundi I, ikiiacha Iraq mkiani bila pointi.
Mbali na Mbappe kuipeleka timu hiyo mtoano, mabao hayo mawili yamemfanya mshambuliaji huyo wa Real Madrid kufikisha 16 katika historia ya Kombe la Dunia, akilingana na mshambuliaji wa zamani wa Ujerumani, Miroslav Klose aliyekuwa kinara wa muda wote wa wafungaji wa mashindano hayo.
Rekodi hiyo ya Klose imekuja kuvunjwa Juni 22, 2026 na Lionel Messi wa Argentina baada ya kufunga mabao mawili kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Austria iliyomfanya nyota huyo kufikisha idadi ya mabao 18.
Kwa sasa unaweza kusema vita imehamia kwa Messi na Mbappe kwani wawili hao wanafukuzana kwa mabao.
Ukiangalia orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika historia ya Kombe la Dunia, Messi ana mabao 18, akimuacha mawili Mbappe.
Pia orodha ya wafungaji bora wa fainali hizo mwaka huu, Messi anaongoza akiwa na mabao matano, akifuatiwa na Mbappe mwenye manne sawa na Erling Haaland.