
Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ubungo imemhukumu fundi ujenzi, Metson Frank (23), maarufu Mkumbo, kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wake wa kambo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi 10.
Frank, mkazi wa Goba ametiwa hatiani kwa kosa la kumlawiti mtoto huyo wa kike katika tukio lililotokea Septemba 10, 2025.
Hukumu hiyo imesomwa leo Alhamisi, Juni 25, 2026 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Tumsifu Barnabas baada ya kuridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka pasipo kuacha shaka yoyote.
Katika uchambuzi wake wa ushahidi, Hakimu Barnabas amesema ushahidi uliotolewa na mashahidi pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo, unaonyesha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo akiwa nyumbani kwa wazazi wake eneo la Goba.
Mahakama imeelezwa kuwa siku ya tukio mama wa mtoto, ambaye alikuwa mjamzito wakati huo, alikwenda kulala chumbani kutokana na hali yake, na mshtakiwa akabaki na mtoto huyo katika chumba kingine.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa, hali ya afya ya mtoto ilianza kubadilika siku iliyofuata na kuendelea kuzorota hadi alipopelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu.
Akichambua ushahidi wa daktari uliowasilishwa na upande wa Jamhuri, Hakimu Barnabas amesema mtoto huyo alifikishwa hospitalini akiwa katika hali mbaya na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Mahakama imeelezwa kuwa uchunguzi wa kitabibu unaonesha dalili za kufanyiwa ukatili huo, hali iliyosababisha taarifa kutolewa kwa Jeshi la Polisi ambalo lilianza uchunguzi na baadaye kumkamata mshtakiwa.
Katika uamuzi wake, Hakimu Barnabas amesema mahakama imejiridhisha na ushahidi wa mashahidi wanane pamoja na vielelezo vitatu vilivyowasilishwa na upande wa mashtaka.
“Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote na kufanya uchambuzi wa kina wa ushahidi uliowasilishwa, mahakama inakutia hatiani kwa kosa la kulawiti kinyume na kifungu cha 154(1) (a)(2) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2023,” amesema Hakimu Barnabas.
Hakimu huyo amemweleza mshtakiwa kuwa ana haki ya kukata rufaa iwapo hajaridhika na uamuzi wa mahakama.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Flora Massawe akisaidiana na mawakili wa Serikali, Agatha Lumato na Clemence Mango, uliomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
“Tunaiomba mahakama yako impe mshtakiwa adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wote wanaojihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto,” amesema Wakili Lumato.
Kwa upande wake, mshtakiwa aliiomba mahakama izingatie maelezo yake kabla ya kutolewa kwa adhabu, akidai hakufahamu chanzo cha hali ya mtoto hadi alipokamatwa na polisi baada ya uchunguzi kukamilika.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Barnabas amekubaliana na maombi ya upande wa Jamhuri.
“Nimezingatia hoja zote zilizowasilishwa mahakamani. Hivyo, ninamhukumu Metson Frank kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa wengine,” amesema.