Arusha. Watu waliowahi kutumia dawa za kulevya na kupona wameiomba Serikali kuongeza juhudi za kudhibiti usambazaji wa dawa hizo, wakionya kuwa kuibuka mpya zinazotengenezwa maabara zinaweza kuhatarisha afya na mustakabali wa vijana.

Tahadhari hiyo imetolewa wakati Ripoti ya Taifa ya Dawa za Kulevya ya mwaka 2025 ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ikionyesha kuwa kwa mara ya kwanza nchini, dawa aina ya Kratom, MDMA na MDA ziligunduliwa na kukamatwa katika operesheni zilizofanyika mwaka jana.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Dawa za Kulevya yaliyofanyika Arusha leo Juni 25, 2026, Mratibu wa Voice of Sober Houses, Hassan Ally amesema dawa za maabara zimeanza kuonekana miongoni mwa watumiaji na zina madhara makubwa zaidi.

“Sasa tunakutana na watumiaji wenye dalili tofauti. Dawa za zamani kama heroini zimepungua kutokana na juhudi za Serikali, lakini dawa za maabara zinazotengenezwa kwa kemikali zimeanza kujitokeza,” amesema Hassan.

Mratibu wa Huduma za Methadone (MAT) katika Hospitali ya Mount Meru, Magreth Elias Msigwa amesema kliniki hiyo imesajili wateja 907 tangu kuanzishwa kwake, huku zaidi ya 130 wakihitimu matibabu na kurejea katika maisha ya kawaida. Amesema takribani wateja 250 wanaendelea na huduma na waraibu 33 wamepoteza maisha.

Kwa niaba ya Kamishna wa DCEA Kanda ya Kaskazini, Ofisa Ustawi wa Jamii, Brenda Mbati amesema kati ya Juni 2025 na Juni 2026, operesheni 227 zilifanyika na watuhumiwa 550 kukamatwa. Pia kilo 5,417.26 za mirungi, kilo 3,010.30 za bangi na gramu 14 za heroini zilikamatwa.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amesema Arusha inapaswa kuwa makini kutokana na hadhi yake kama kitovu cha utalii na mikutano ya kimataifa.

Naye Flora Manongi aliyewahi kuwa mraibu wa dawa za kulevya ameitaka jamii kuacha kuwanyanyapaa waliopona na badala yake kuwasaidia kujenga upya maisha yao.

Maadhimisho hayo yalifanyika chini ya kaulimbiu isemayo, “Ubunifu wa Kimkakati: Suluhisho la Changamoto za Dawa za Kulevya.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *