Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei ametoa wito kwa Mahakama ya Iran kufuatilia na kurejesha haki za taifa ambazo zimekiukwa kutokana na vita vya uchokozi vya Marekani na Israel tangu mwaka jana.

Katika ujumbe wake uliotolewa leo Jumapili katika kumbukumbu ya kuuawa shahidi Ayatullah Muhammad Beheshti na wenzake, inayoadhimishwa kama Wiki ya Mahakama, Ayatullah Khamenei amesema mojawapo ya masuala muhimu zaidi ya kisheria na kimahakama yanayolikabili taifa zima la Iran kwa sasa ni kufuatilia na kurejesha haki hizo zilizokiukwa na “wahalifu wa kimataifa na mataifa ya kibeberu na chokozi.”

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba kulinda haki za watu wa Iran kunavuka masuala ya kisheria ya mtu binafsi na kunajumuisha kutetea haki za pamoja za nchi dhidi ya uhalifu unaofanywa na wavamizi wa kigeni.

Amesema Idara ya Mahakama katika Jamhuri ya Kiislamu ina jukumu la kulinda haki za watu, kuhuisha haki za umma na uhuru halali, kupambana na ufisadi, kutekeleza haki, kutetea sheria za Mwenyezi Mungu, na kusimamia utekelezaji wa sheria.

Amesisitiza kuwa, mafanikio katika kutekeleza majukumu hayo yataimarisha imani ya umma katika mfumo wa mahakama.

Akizungumzia changamoto kubwa zaidi ya kisheria nchini, Ayatullah Khamenei amesema kufuatilia haki zilizokiukwa na wahalifu na wavamizi wa kimataifa, hasa tangu mwaka jana, ni miongoni mwa majukumu muhimu ya Idara ya Mahakama.

Amesema damu ya wale waliouawa katika vita viwili vya uchokozi dhidi ya Iran – vilivyoanzishwa na Marekani na Israel mnamo Juni 2025 na Februari 2026 – pamoja na madhara ya kimwili, kisaikolojia na kiroho yaliyosababishwa kwa Iran na watu wake ndani na nje ya nchi, ndio msingi wa mamia au hata maelfu ya kesi muhimu za kisheria.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameashiria mauaji ya watoto na uhalifu wa kivita ambao haujawahi kutokea uliofanywa na Marekani na Israel huko Minab na Lamerd, mashambulizi dhidi ya vituo vya matibabu na huduma za umma, na mauaji raia kuanzia watoto wachanga hadi wazee.

Zaidi ya yote, ameashiria kuuliwa shahidi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ambaye amemtaja kama “mtu asiye na kifani, kito cha kipekee cha zama za sasa, na kiongozi mkuu wa Mujahidina,” akisema kila kesi lazima ifuatiliwe kwa uzito mbele ya mahakama za ndani na za kimataifa.

“Kilicho hakika ni kwamba wahalifu lazima wafikishwe mbele ya sheria na kuadhibiwa kwa matokeo ya vitendo vyao vya uhalifu,” amesema Sayyid Khamenei.

Amesisitiza kuwa, hatua kama hizo za kisheria zitasaidia kuzuia kurudiwa uhalifu kama huo katika siku zijazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *