
Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran limetangaza kuwa wahusika wa uhalifu na mauaji dhidi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei na watu wa Iran watakabiliwa na adhabu “kwa wakati unaofaa” kutoka kwa “viumbe waadilifu,” huku nchi hii ikijiandaa kwa mazishi ya Imam Sayyid Ali Khamenei.
“Ngumi iliyokunjwa ya Kiongozi aliyeuawa shahidi wakati wa kupaa kwake na kurejea kwa Mola itabaki kuwa ishara ya kudumu ya mafundisho na sera ya usalama wa taifa ya Iran,” amesema Mohammad Baqer Zolqadr, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran.
Zolqadr, kamanda mkongwe wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) aliyeteuliwa katika nafasi ya juu ya usalama wa taifa mnamo Machi 24 mwaka huu baada ya mauaji ya mtangulizi wake, Ali Larijani katika shambulio la Marekani na Israel, ametoa onyo hilo kabla ya shughuli ya mazishi ya Imam Khamaeni inayotarajia kuanza siku kadhaa zijazo.
“Faili la kulipiza kisasi cha damu safi ya Khamenei Muadhamu na mashahidi waliodhulumiwa wa Iran bado liko wazi,” ametangaza Zolqadr na kuongeza: “Wahalifu na wale walioamuru uhalifu huo watakabiliwa na adhabu yao ya haki kutoka kwa ‘viumbe waadilifu, kwa wakati unaofaa—ambao hautachukua muda mrefu—.”
Katika taarifa tofauti, Baraza la Walinzi wa Katiba nchini Iran, limesema adui alitenda “uhalifu huo mbaya” kwa matumaini ya uongo ya kuvunja irada na azma ya taifa la Iran.
“Lakini hawakujua kwamba kuuawa shahidi Kiongozi Muadhamu kutakuwa tochi ya mapambano na Muqawama na mwongozo wa ushindi,” imesema taarifa hiyo.
Baraza hilo limeyataja mazishi ya Kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni “kipindi cha kihistoria cha mabadiliko” katika uthabiti wa mfumo wa Kiislamu, na kuongeza kwamba damu safi ya Kiongozi Mkuu itaangazia njia ya ukweli hadi ushindi wa mwisho utakapopatikana na itazidi kuikatisha tamaa kambi ya ubeberu.
“Mazishi haya si shughuli ya maombolezo tu, bali ni dhihirisho la imani na uaminifu wa taifa ambalo, kwa miaka mingi chini ya uongozi wa Ayatullah Khamenei, limepita katika njia ya heshima na Muqawama. Shughuli hii kubwa ni ishara ya nguvu ya Iran dhidi ya kambi ya ubeberu na fursa ya kutangaza tena utiifu kwa maadili ya Mapinduzi,” imesema taarifa ya Baraza la Walinzi wa Katiba.
“Watu wa Iran, kwa mahudhurio yao makubwa, wataonyesha mshikamano na umoja wa kitaifa,” imesisitizia taarifa hiyo na kuongeza: “Watatuma ujumbe kwa ulimwengu mzima kwamba kuuawa shahidi Kiongozi wao kumeimarisha zaidi azma ya taifa.”