
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewaita wataalamu watatu wabobezi wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC), Mwanza, na Wizara ya Afya, Dodoma, kufanya uchunguzi wa kina wa mwili wa Suezi Maradufu ili kuondoa sintofahamu iliyogubika kuhusu kifo chake.
Maradufu, aliyekuwa dereva wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, alifariki dunia usiku wa kuamkia jana, Jumatano, Julai mosi, 2026, mkoani Kigoma. Mwili wake ulikutwa ndani ya chumba katika nyumba ya kulala wageni ya Ntahamba, alikokuwa amefikia.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Julai 2, 2026, kutoka Kigoma, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Aman Golugwa, amesema wamewaita wataalamu hao kwa sababu wanaamini uchunguzi wa kina unahitaji wataalamu wenye uzoefu maalumu ambao hawapo Hospitali ya Mkoa wa Kigoma.
“Wataalamu wawili kutoka Bugando wamewasili, huku tukimsubiri mtaalamu mwingine kutoka Wizara ya Afya, Dodoma. Tunatarajia uchunguzi ufanyike leo ili kuanzia saa saba mchana tuanze safari ya kuelekea Tarime, mkoani Mara, kwa ajili ya mazishi,” amesema Golugwa.
Jana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma lilithibitisha kutokea kwa kifo hicho kupitia taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, polisi walipokea taarifa kutoka kwa Mrimi Zabron Mwita, Katibu wa Heche, aliyesema walifika katika nyumba ya kulala wageni ya Ntahamba kumuamsha Maradufu baada ya kumpigia simu kwa muda mrefu bila mafanikio, huku wakitaka kuendelea na ratiba yao ya safari.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa askari polisi walifika katika nyumba hiyo ya wageni wakiambatana na Mrimi pamoja na wafanyakazi wa nyumba hiyo na kuonyeshwa chumba alichokuwa amelala Maradufu.
“Askari walikuta mlango wa chumba umefungwa, hivyo walilazimika kuuvunja mbele ya mashuhuda waliotoa taarifa kwamba hawakuweza kumpata kwa njia ya simu. Baada ya mlango kufunguliwa, walimkuta Suezi Dani Maradufu akiwa amelala chini kifudifudi,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa polisi, uchunguzi wa awali ulibaini kuwa ndani ya chumba hicho kulikuwa na dawa mbalimbali za matumizi ya binadamu. Mwili wa marehemu ulihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni kwa uchunguzi zaidi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amesema awali walitaka kufanya uchunguzi wa maiti (postmortem) wa mwili huo, lakini Chadema walikuwa na wasiwasi na walitaka kuleta wataalamu wake ili wafanye kazi pamoja na wale wa Serikali kwa lengo la kuondoa sintofahamu.
“Ingawa kwa uzoefu wa askari wetu kifo chake kinaonekana kuwa cha kawaida, lakini kwa kuwa jambo hili limechanganyika na masuala ya kisiasa, tunasita kudhani kuna mkono wa mtu,” amesema.
Amesema wataalamu wa Chadema pamoja na wale wa Serikali watafanya uchunguzi, kisha watatoa majibu baada ya kuyachambua ili kuondoa sintofahamu iliyojitokeza.
Katika hatua nyingine, Golugwa amesema Chadema inaendelea kufanya maandalizi yote muhimu huku ikiwasiliana kwa karibu na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk Joseph Nangawe, ili kuhakikisha uchunguzi wa maiti (postmortem) unaanza mara tu wataalamu wote watakapokamilisha kuwasili.
“Tunataka kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili kubaini nini hasa kimesababisha kifo chake. Mazingira ya kifo chake yana utata kwa sababu hakuwa mgonjwa, lakini mwili wake ulikutwa ukiwa unavuja damu puani, masikioni na mdomoni.
“Tulimkuta amelala sakafuni huku damu zikimtoka masikioni. Katika mazingira ya kawaida, hali hiyo inaleta maswali mengi. Inawezekana alikula au alikunywa kitu, kwa sababu alikuwa peke yake chumbani.”
Golugwa amesema ni muhimu uchunguzi ukafanyika kwa kina ili kuondoa kila aina ya shaka, akisisitiza kuwa Maradufu hakuwa na historia ya ugonjwa wowote waliofahamu.
“Alikuwa na dawa kama Azuma, Action na Flagyl. Hizi ni dawa za kawaida ambazo mtu yeyote anaweza kuwa nazo akiwa safarini. Hata mimi kwenye begi langu nina dawa mbalimbali za maumivu, lakini Maradufu hakuwahi kutuambia kwamba alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wowote,” amesema.
Kwa mujibu wa Golugwa, mazingira ya kifo hicho yanaendelea kuibua maswali, hasa kutokana na hali ya marehemu kukutwa damu zikitoka mdomoni, masikioni na puani, jambo analosema si la kawaida.
“Tukishapata majibu ya uchunguzi, tutatoa taarifa rasmi. Uchunguzi wa maiti unaweza kuanza wakati wowote kuanzia sasa,” amesema.