Chanzo cha picha, Getty Images
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7
Ajali ya hivi karibuni ya ndege ya kurusha mabomu la Jeshi la Anga la Marekani aina ya B-52 kusini mwa California imeirejesha ndege hii maarufu katika historia kwenye macho ya umma.
Ndege hiyo, iliyopata ajali muda mfupi baada ya kupaa kutoka Kituo cha Jeshi la Anga cha Edwards, haikuwa tu ndege ya kijeshi katika mazoezi, ila ni ndege maalum ya krusha mabomu linalohusishwa na Vita Baridi, uzuiaji wa silaha za nyuklia, na imeshiriki katika vita vikuu vya Marekani kuanzia Vietnam hadi Iraq na Afghanistan.
Katika Jangwa la Mojave la California, baadhi ya ndege za kijeshi za Marekani zilizo na teknolojia ya juu na zilizoishi kwa muda mrefu hufanyiwa majaribio.
Hapa tunazungumzia ndege zilizoundwa zaidi ya miaka sabini iliyopita, lakini inatumika na vikosi vya operesheni vya Jeshi la Anga la Marekani.
Ndege aina ya B-52, iliyotengenezwa miaka ya 1950, bado inaendelea kuboreshwa ili iendelee kutumika vitani.
Baadhi ya maboresho hayo yanajumuisha mifumo ya rada, urambazaji, na silaha.
Ndege hiyo iliyopata ajali ilikuwa na watu wanane ambao wote walifariki.
Historia ya B-52
Ndege ya kurusha mabomu aina ya B-52 ilitengenezwa kmiaka ya 1950, wakati wa kilele cha mashindano ya silaha kati ya Marekani na Umoja wa Kisovyeti wakati wa Vita Baridi.
Lengo la kutengenezwa kwake ilikuwa iwe ndege inayoweza kusafiri umbali mrefu sana, kubeba idadi kubwa ya mabomu, yakiwemo silaha za nyuklia, na kushambulia malengo yaliyoko ndani kabisa ya eneo la adui.
Ndege hii ilianza kutumika rasmi mwaka 1955, na tangu wakati huo imekuwa mojawapo ya alama kuu za nguvu za anga za Marekani kutokana na uwezo wake mkubwa wa kushambulia, kuruka masafa marefu, na kubeba kiasi kikubwa cha silaha kwa umbali mrefu.
Jina lake kamili, Stratofortress, kumaanisha “Ngome ya Kimkakati.” Jina hili linaonyesha jukumu ambalo B-52 ilibuniwa kulitekeleza wa kubeba mabomu makubwa katika masafa marefu, kufanya mashambulizi na kuzuia mashambulizi ya nyuklia.
Kwa muundo wake mkubwa, mabawa marefu na injini nane, B-52 imekuwa mojawapo ya ndege za kijeshi zinazotambulika zaidi duniani kutokana na mwonekano wake, sauti yake na uwepo wake angani.
Wakati wa Vita Baridi, B-52 ilikuwa sehemu muhimu ya mkakati wa Marekani wa kuzuia vita vya nyuklia. Wakati huo, dunia ilikuwa na hofu ya kutokea kwa mapambano ya moja kwa moja kati ya Washington na Moscow. Hata hivyo, jukumu la ndege hiyo halikuishia kwenye kuzuia vitisho vya nyuklia pekee.
Baadaye, B-52 ikawa mojawapo ya silaha kuu za Marekani katika vita vya kawaida, kuanzia Vita vya Vietnam ambako ilitumika kwa kiwango kikubwa tangu miaka ya 1960, hadi Vita vya Ghuba ya Uajemi mwaka 1991, vita vya Afghanistan baada ya mwaka wa 2001, uvamizi wa Iraq mwaka 2003, na katika miaka iliyofuata ilitumika pia katika operesheni dhidi ya kundi la kigaidi la ISIS nchini Syria na Iraq tangu mwaka 2014.
Marekani imeendelea kuitunza ndege hii kwa sababu ya uwezo wake wa kuendelea kuboreshwa. Ndege ya B-52 ilitengenezwa kuwa na uwezo wa kubeba silaha nyingi na kusafiri umbali mrefu.
Kwa miongo kadhaa, Marekani imekuwa ikiboresha mifumo ya ndani ya ndege hiyo.
Maboresho hayo yanahusisha mifumo ya urambazaji, mawasiliano, rada, vifaa vya vita vya kielektroniki, pamoja na aina za silaha ambazo B-52 inaweza kubeba.
Ingawa ukubwa wake unaweza kuonekana kuwa hasara katika enzi ya sasa ya ndege zisizoonekana kwa urahisi kwenye rada, pia inatoa faida muhimu, B-52 inaweza kubeba aina mbalimbali za silaha katika misheni moja.
Kutokana na hilo, Washington haiioni B-52 kama ndege ya zamani tu bali Inaiona kama mfumo unaoweza kuendelea kuboreshwa na kuwekewa teknolojia mpya kadri mbinu za vita zinavyobadilika.
Hii ndiyo maana B-52 bado inaendelea kutumika katika Jeshi la Anga la Marekani licha ya kuvumbuliwa kwa ndege za kisasa za kurusha mabomu kama B-1 na B-2, huku Marekani ikiendelea kutengeneza ndege zingine mpya za kurusha mabomu.
B-52 ina uwezo gani wa kijeshi?
Chanzo cha picha, Getty Images
Umuhimu wa B-52 unaonekana wazi zaidi tunapoangalia uwezo wake kwa takwimu. Ndege hii kubwa inaweza kuruka masafa kwa masafa marefu kupitia mabara tofauti na ina uwezo wa kusafiri maelfu ya kilomita bila kujazwa mafuta angani. Ndege hiyo pia inaweza kuongezwa mafuta ikiwa angani.
B-52 hutumia injini nane, jambo linaloiwezesha kubeba mzigo mkubwa wa silaha, ukiwemo zaidi ya tani 31 za mabomu na makombora.
Ndege hiyo inaweza kubeba silaha za kawaida zinazoongozwa kwa usahihi, zikiwemo mabomu na makombora ya masafa marefu. Pia imeundwa kubeba silaha za nyuklia kama sehemu ya mkakati wa Marekani wa kuzuia vitisho vya nyuklia.
Kwa kawaida, wafanyakazi wake ni watano, wakiwemo rubani, rubani msaidizi, pamoja na maafisa wanaosimamia urambazaji, mifumo ya silaha na vita vya kielektroniki.
Licha ya ukubwa wake wa nje, sehemu ya ndani ya B-52 si ya starehe kama wengi wanavyoweza kudhani. Ndani yake hufanana zaidi na kituo cha operesheni za kijeshi, ikiwa imejaa vifaa, skrini za ufuatiliaji na mifumo ya udhibiti.
Ndege hii hupaa juu sana angani na inaweza kubaki angani kwa saa nyingi, jambo linalolifanya lifae kwa misheni za masafa marefu na operesheni ngumu.
Hata hivyo, B-52 si ndege ya teknolojia ya kisasa, hivyo haijaundwa ili isionekane kwenye rada. Badala yake, uwezo wake unategemea masafa yake marefu, uwezo mkubwa wa kubeba silaha, matumizi ya silaha za usahihi zinazoweza kushambulia kutoka mbali, pamoja na usaidizi wa mtandao mpana wa operesheni za anga unaojumuisha ndege za kivita, ndege za upelelezi na ndege za kujaza mafuta angani.
B-52 imeshiriki katika vita gani?
B-52 haikuwa tu alama ya mkakati wa kuzuia vita vya nyuklia wakati wa Vita Baridi, bali pia imeshiriki katika baadhi ya vita na operesheni muhimu zaidi za kijeshi za Marekani tangu miaka ya 1960.
Ushiriki mkubwa zaidi wa B-52 vitani ulikuwa katika Vita vya Vietnam. Marekani ilitumia ndege hiyo kushambulia kwa mabomu ngome za majeshi ya Vietnam, njia za usambazaji na malengo mengine ya kijeshi kwa kiwango kikubwa. Jina la B-52 lilihusishwa sana na mbinu inayojulikana kama “carpet bombing”, yaani kurusha idadi kubwa ya mabomu juu ya eneo pana kwa wakati mmoja, mojawapo ya mbinu kali na zenye utata katika vita vya anga.
Baadaye, B-52 ilitumika kwa kiwango kikubwa katika Vita vya Ghuba ya Uajemi mwaka 1991, wakati wa Operesheni Desert Storm dhidi ya Iraq. Katika vita hivyo, ilitekeleza mashambulizi ya masafa marefu, baadhi yake yakianzishwa kutoka vituo vya kijeshi ndani ya Marekani. Ndege hizo zilijazwa mafuta angani, zikashambulia malengo nchini Iraq, kisha zikarejea au kutua katika vituo vingine vya kijeshi.
Mwishoni mwa miaka ya 1990, B-52 ilishiriki katika operesheni za anga dhidi ya iliyokuwa Yugoslavia na Kosovo kama sehemu ya kampeni ya NATO.
Baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001, ndege hiyo ilitumika tena nchini Afghanistan, ambako ilitoa msaada wa mashambulizi ya mabomu.
B-52 pia ilishiriki katika Vita vya Iraq mwaka 2003, na baadaye katika operesheni dhidi ya kundi la kigaidi la ISIS nchini Iraq na Syria.
B-52 imetekeleza zaidi ya jukumu lake la awali la kuwa chombo cha kuzuia vitisho vya nyuklia dhidi ya Umoja wa Kisovyeti na kuwa mojawapo ya nyenzo muhimu za Marekani katika vita vya kawaida, mashambulizi ya masafa marefu na operesheni za kutoa msaada wa anga.
B-52 ina uhusiano gani na mkakati wa kuzuia vita vya nyuklia?
B-52 inahusishwa kwa karibu na mkakati wa Marekani wa kuzuia vita vya nyuklia. Ndege hii ilibuniwa awali kuwa sehemu ya uwezo wa Marekani wa kufanya mashambulizi ya masafa marefu iwapo kungezuka vita vikubwa vya nyuklia kati ya Marekani na Umoja wa Kisovyeti wakati wa Vita Baridi.
Mkakati wa kuzuia vita vya nyuklia haumaanishi lazima kutumia silaha za nyuklia, bali unalenga kumfanya adui aamini kwamba shambulio lolote la nyuklia litajibiwa kwa mashambulizi makubwa na yenye madhara makubwa. Kwa sababu hiyo, Marekani ilihitaji njia mbalimbali za kufikisha silaha za nyuklia, zikiwemo makombora ya masafa marefu ya manowari za nyuklia, na ndege za kurusha mabomu ya kimkakati ya masafa marefu kama B-52.
Ndege kama B-52 ina jukumu tofauti na vyombo vingine vya makombora au manowari. Kombora la masafa marefu hurushwa kwa kasi kubwa sana na haliwezi kusimamishwa baada ya kurushwa. Kwa upande mwingine, bomu iliyorushwa na B-52 linaweza kubaki angani kwa muda, na kuelekezwa kwenye shabaha nyingine, au hata kurejeshwa kabla kabla ya kutekeleza mashambulizi.
Uwezo huu wa kubadilika huifanya B-52 kuwa si tu chombo cha kijeshi, bali pia nyenzo ya kisiasa, kwa kuwa inaweza kutuma ujumbe wa wazi wa kuzuia adui.

Mchango wa kampuni ya Boeing kwa B-52
Jina la B-52 linahusishwa na kampuni ya Boeing, ambayo iliibuni na kuitengeneza ndege hiyo kwa ajili ya Jeshi la Anga la Marekani katika miaka ya 1950. Wakati huo, Washington ilikuwa ikitafuta ndege ya kimkakati yenye uwezo wa kubeba silaha za nyuklia na kufikia malengo ya mbali wakati wa Vita Baridi.
Hata hivyo, uhusiano wa Boeing na B-52 haukuishia katika hatua ya utengenezaji. Zaidi ya miongo saba baadaye, kampuni hiyo imeendelea kushiriki katika maboresho ya ndege hiyo kwa kuifanyia maendeleo ya mifumo ya kisasa ya rada, mawasiliano na silaha ili iweze kuendelea kutumika katika kikosi cha operesheni cha Jeshi la Anga la Marekani.
B-52 imebadilika kutoka kuwa chombo cha zamani cha kijeshi na kuwa mradi unaoendelea wa kuongeza maisha ya huduma ya mojawapo ya ndege muhimu zaidi katika anga za Marekani.
Ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zinaonyesha kuwa ndege iliyopata ajali hivi karibuni ilikuwa ikitekeleza misheni ya majaribio iliyohusiana na mpango wa kuboresha mfumo wake wa rada.