
Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani, ameliandikia barua Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa umoja huo kufuatia uchokozi wa Marekani dhidi ya Iran, kushambuliwa miundombinu na mauaji ya raia wa Iran.
Iravani amesema Washington imekamilisha uhalifu wake wa kivita dhidi ya watu wa Iran kutokana na kutochukua hatua Baraza la Usalama, akielezea jambo hilo kuwa ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa ya kibinadamu.
Iravani amenukuu takwimu za Wizara ya Afya ya Iran, akisema kwamba tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Julai, hadi asubuhi ya Julai 17, raia 43 wa Iran walikuwa wameuawa na wengine 400 kujeruhiwa.
Miongoni mwa waliouawa walikuwa wanawake watatu na mtoto mmoja, huku wanawake 22 na watoto tisa wakiwa miongoni mwa waliojeruhiwa.
Iravani amesema uchokozi wa Marekani, uliofanywa kati ya usiku wa Julai 16 na mapema Julai 17, ulilenga maeneo ya jimbo la Hormozgan na kusababisha vifo vya raia na uharibifu wa kimfumo wa miundombinu ya raia kupitia uharibifu wa madaraja makubwa.
Ametaja uhalifu mwingine uliofanywa na Marekani, akisema kwamba baada ya moja ya madaraja kuharibiwa, gari la raia lilianguka kutoka juu ya daraja lililoharibiwa na kusababisha vifo vya raia saba na wengine tisa kujeruhiwa.
Iravani amesema kwamba jeshi la Marekani limelenga moja kwa moja miundombinu ya reli ya raia, na kushambulia kituo cha reli cha Bandar Abbas, kituo muhimu kusini mwa Iran kinachounganisha Bandari ya Shahid Rajaee na kutumika kama kitovu muhimu cha Ukanda wa Usafiri wa Kimataifa wa Kaskazini-Kusini.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba kulengwa mara kwa mara kwa mali na maeneo ya raia, hasa mitandao muhimu ya usafiri na mifumo ya reli, ni uhalifu wa kivita. Amesema Marekani inawajibika kikamilifu kimataifa kwa mauaji, kujeruhi, uharibifu wa miundombinu, uharibifu wa mazingira na uharibifu wote unaosababishwa na “vitendo vyake kinyume cha sheria kimataifa.”
Kwa kuzingatia hayo yote, Iravani amesema Iran imetoa wito kwa Baraza la Usalama kutimiza wajibu wake wa msingi chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kudumisha amani na usalama wa kimataifa na kuchukua hatua za haraka na madhubuti za kukomesha uchokozi wa Marekani na kuhakikisha inawajibishwa kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Amemalizia kwa kusisitiza kwamba kutochukuliwa hatua yoyote madhubuti ya Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kunaihalalishia Jamhuri ya Kiislamu haki yake ya asili chini ya sheria za kimataifa ya kuchukua hatua zote muhimu ili kulinda mamlaka yake, ardhi, watu na maslahi muhimu ya kitaifa.