
Uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kutosaini hati yoyote ya utekelezaji wa hukumu za kifo tangu alipoingia madarakani, umefungua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa adhabu hiyo nchini, huku baadhi ya wadau wakitaka ifutwe kwa madai kuwa ni adhabu ya kikatili inayokiuka haki ya msingi ya binadamu ya kuishi.
Akizungumza na mawakili wa Serikali jijini Arusha hivi karibuni, Rais Samia alisema tangu achukue nafasi ya urais hajawahi kusaini hati ya kifo (death warrant) kwa ajili ya kutekeleza hukumu kwa wafungwa waliokutwa na hatia na kuhukumiwa kunyongwa.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, adhabu ya kifo bado ipo katika mfumo wa sheria na utekelezaji wake unahitaji uamuzi wa mwisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Hata hivyo, kutosaini hati hizo kumeonekana na baadhi ya wadau kama hatua inayosaidia kulinda maisha ya watu huku ikitoa nafasi ya kutafakari upya umuhimu wa kuendelea kuwapo kwa adhabu hiyo.
Wanaotaka kufutwa kwa adhabu hiyo wanahoji kuwa haki ya kuishi ni haki ya msingi inayotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kupitia Ibara ya 14.
Hata hivyo, wanabainisha kuwa sheria za makosa ya jinai zimeendelea kuweka adhabu ya kifo kwa makosa mbalimbali ikiwamo mauaji, uhaini, ugaidi na makosa ya usaliti wakati wa vita.
Kwa mtazamo wao, hali hiyo inaleta mgongano kati ya wajibu wa kulinda haki ya kuishi na uwepo wa sheria inayoruhusu kuondolewa kwa maisha ya mtu baada ya hukumu ya mahakama.
Wadau hao wanasema adhabu ya kifo haiwezi kusaidia kurekebisha makosa endapo mtu atahukumiwa kimakosa, kwa kuwa utekelezaji wake ukishafanyika hakuna namna ya kurejesha maisha ya mtu huyo. Wanasema changamoto za mifumo ya haki jinai katika nchi mbalimbali zimewahi kusababisha watu kuhukumiwa na baadaye kubainika kuwa hawakuwa na hatia.
Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi ambazo hazijatekeleza adhabu ya kifo kwa muda mrefu, ambapo mara ya mwisho hukumu hiyo kutekelezwa ilikuwa mwaka 1994. Kwa zaidi ya miaka 30 sasa, wafungwa waliopo kwenye hukumu za kifo wameendelea kubaki gerezani bila utekelezaji wa hukumu hiyo.
Tangu Tanzania ipate uhuru, zaidi ya watu 700 wamewahi kuhukumiwa kifo, ingawa idadi ya waliotekelezewa hukumu hizo ni ndogo. Katika awamu mbalimbali za uongozi, baadhi ya marais wamechukua hatua tofauti kuhusu suala hilo, wakiwamo waliotoa misamaha kwa wafungwa waliokuwa kwenye hukumu hizo.
Katika awamu ya kwanza ya uongozi wa Taifa, Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, anatajwa kusaini baadhi ya hati za utekelezaji wa hukumu za kifo, huku viongozi waliofuata wakionyesha mitazamo tofauti kuhusu matumizi ya adhabu hiyo.
Wanaopinga kuendelea kuwapo kwa adhabu hiyo pia wanahoji kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha kuwa adhabu ya kifo inapunguza makosa makubwa yanayosababisha kutolewa kwa hukumu hiyo. Wanatoa mfano wa baadhi ya nchi ambazo zimeendelea kuwa na adhabu hiyo lakini bado zinakabiliwa na matukio ya mauaji.
Aidha, wanasisitiza kuwa waathirika wakubwa wa mfumo huo mara nyingi ni watu wasio na uwezo wa kifedha wa kupata msaada wa kisheria wa kiwango cha juu, jambo linaloweza kuongeza hatari ya watu wasio na hatia kupewa adhabu isiyoweza kurekebishwa.
Mbali na athari kwa mtu anayehukumiwa, wadau hao wanaeleza kuwa adhabu ya kifo huacha madhara makubwa kwa familia za wahusika, hususani watoto wanaobaki bila wazazi au walezi wao.
Hata hivyo, wapo wanaosisitiza kuwa kwa makosa makubwa yanayosababisha madhara makubwa kwa jamii, adhabu kali zinahitajika ili kuhakikisha haki inatendeka kwa waathirika na kuzuia watu wengine kufanya makosa kama hayo.
Pamoja na mitazamo hiyo tofauti, mjadala kuhusu adhabu ya kifo unaendelea huku kukiwa na wito kwa Serikali na jamii kwa ujumla kutafakari upya nafasi ya adhabu hiyo katika mfumo wa haki nchini.
Baadhi ya wadau wameitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kutoa misamaha kwa baadhi ya wafungwa waliopo kwenye hukumu za kifo na kuhakikisha suala hilo linapatiwa nafasi katika mchakato wowote wa marekebisho ya Katiba.
Kwao, hatua ya viongozi kutosaini hati za kifo inaonekana kuwa ishara ya mwelekeo unaoweka mbele thamani ya maisha ya binadamu, huku mjadala mkubwa ukiwa sasa ni namna Tanzania itakavyoamua hatima ya adhabu hiyo katika siku zijazo.