Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameipa Kampuni ya Wakazi inayomiliki leseni ya uchimbaji wa dhahabu katika Kijiji cha Chirorwe, wilayani Musoma, siku moja kuhakikisha inailipa familia ya Ruhumbika Machumu fidia ya Sh40 milioni ili iondoke katika eneo hilo na kupisha shughuli za uchimbaji.
Sambamba na agizo hilo, Kanali Mtambi amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kutoa usafiri wa kuihamisha familia hiyo kutoka eneo la machimbo kwenda makazi mapya yaliyotengwa kwa ajili yao.
Ametoa maagizo hayo leo, Jumatano, Julai 22, 2026, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Chirorwe, uliolenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na wachimbaji wadogo wa dhahabu.
Hatua hiyo imekuja baada ya mgogoro wa zaidi ya miaka miwili kati ya familia hiyo na wachimbaji wadogo kuhusu fidia ya ardhi iliyopo ndani ya eneo la uchimbaji kushindwa kupatiwa suluhu.
Baadhi ya wachimbaji wadogo pamoja na wakazi wa Kijiji cha Chirorwe wilayani Musoma wakiwa kwenye mkutano wa hadhara kwaajili ya kusikilizwa kero zao na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi. Picha na Beldina Nyakeke
Baada ya kusikiliza pande zote, Kanali Mtambi amesema kuendelea kwa familia hiyo kuishi katikati ya eneo la uchimbaji ni hatari kwa usalama wao na pia kunakwamisha shughuli za uzalishaji.
“Pamoja na kutumia sheria zinazoongoza masuala ya uchimbaji na umiliki wa ardhi, tunapaswa pia kutumia busara na diplomasia katika masuala yanayogusa maisha ya watu na maendeleo ya uchumi. Tunataka familia iishi katika mazingira salama, lakini pia shughuli za uchimbaji ziendelee bila vikwazo,” amesema.
Amesema familia hiyo inamiliki eneo hilo kihalali, hivyo inastahili kulipwa fidia kabla ya kuondoka ili kupisha shughuli za uchimbaji wa madini.
“Haiwezekani familia iendelee kuishi katika eneo ambalo sasa limezungukwa na shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Ni hatari kwao na pia inapunguza ufanisi wa uzalishaji,” amesema.
Kanali Mtambi amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Musoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuhakikisha ifikapo saa sita mchana kesho, Julai 23, 2026, fedha hizo zimeingizwa kwenye akaunti ya familia hiyo na utaratibu wa kuhama uwe umekamilika.
“Nataka nipate taarifa kuwa Sh40 milioni zipo kwenye akaunti ya familia na maandalizi ya kuhama yamekamilika. Ikiwezekana wahame leo kwa sababu nimeelezwa nyumba ya kuishi tayari imepatikana,” amesema.
Aidha, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Mara kufanya tathmini ya gharama zinazohitajika kufikisha umeme katika eneo hilo ili kuboresha shughuli za wachimbaji wadogo.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wadogo, Damian Nyantora amesema jitihada za kumaliza mgogoro huo zilikwama baada ya familia kubadili msimamo kuhusu kiwango cha fidia.
“Tulikuwa tumekubaliana kuwalipa Sh40 milioni na kuwatafutia nyumba ya kuishi, lakini wakati wa kulipa wakadai wanataka Sh95 milioni, jambo lililotuacha katika sintofahamu,” amesema.
Amesema familia hiyo pia ilitaka kulipwa Sh40 milioni huku ikiendelea kudai umiliki wa eneo hilo baada ya kuhama, hali iliyochelewesha kufikiwa kwa makubaliano.
Kwa upande wake, msemaji wa familia hiyo, Sefaret Ruhumbika, amesema familia imekubali kupokea Sh40 milioni na kuondoka baada ya malipo kukamilika.
Amesema familia hiyo yenye watu 11 inamiliki ekari mbili za ardhi katika eneo hilo pamoja na nyumba mbili za makazi, lakini imeamua kuondoka kutokana na mazingira ya sasa kutokuwa salama.
“Tumekaa kama familia na kukubaliana kupokea Sh40 milioni. Tuko tayari kuhama mara tu tutakapolipwa haki yetu kwa sababu hata sisi hatufurahii kuendelea kuishi katika mazingira haya hatarishi,” amesema.
Ruhumbika amesema awali walishindwa kufikia mwafaka kutokana na kutokuwepo kwa makubaliano ya maandishi kuhusu fidia, lakini wamekubali uamuzi wa mkuu wa mkoa baada ya kuhakikishiwa kuwa malipo yatafanyika kwa utaratibu rasmi.
“Tulikuwa na wasiwasi kwa sababu kulikuwa na mazungumzo yasiyo na maandishi. Sasa tumeridhika baada ya mkuu wa mkoa kutuhakikishia malipo na mkataba unaandaliwa, hivyo tuko tayari kuhama,” amesema.