Dar es Salaam. Ufaransa imeandika historia kwa kuwa moja ya mataifa ya kwanza barani Ulaya kupitisha sheria inayowazuia watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 kutumia mitandao ya kijamii.

Hatua hiyo inayolenga kuwalinda dhidi ya madhara yanayohusishwa na matumizi ya majukwaa ya kidijitali. Kwa mujibu wa DW.

Bunge la nchi hiyo limeidhinisha muswada wa sheria uliokuwa ukisukumwa na Rais Emmanuel Macron, ambaye amesema utekelezaji wake utaanza Septemba mwaka huu.

Chini ya sheria hiyo, watoto walio chini ya umri huo hawataruhusiwa kufungua au kutumia akaunti kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii bila kufuata masharti mapya yaliyowekwa na serikali.

Akizungumza baada ya kupitishwa kwa muswada huo, Macron amesema uamuzi huo ni sehemu ya ahadi zake za kuimarisha ulinzi wa watoto dhidi ya athari za ulimwengu wa kidijitali.

“Ufaransa inaongoza njia barani Ulaya linapohusika suala la kuwalinda watoto na vijana balehe,” amenukuliwa akisema.

Hatua ya Ufaransa inakuja wakati mataifa mengi duniani yakiongeza shinikizo kwa kampuni za teknolojia kuhakikisha watoto wanatumia mitandao kwa usalama zaidi, huku tafiti zikionesha ongezeko la changamoto za afya ya akili, uraibu wa matumizi ya simu na kukumbana na maudhui yasiyofaa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), matumizi ya mitandao ya kijamii na vifaa vya kidijitali  kupita kiasi kwa watoto na vijana yamehusishwa na kuongezeka kwa msongo wa mawazo, wasiwasi, matatizo ya usingizi na kupungua kwa umakini darasani. Shirika hilo linashauri wazazi na serikali kuweka mazingira salama ya matumizi ya teknolojia kwa watoto.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) linaeleza kuwa ingawa mitandao ya kijamii inaweza kusaidia watoto kujifunza na kuwasiliana, matumizi yake bila uangalizi yanaweza kuwaweka katika hatari ya unyanyasaji mtandaoni, uonevu wa kidijitali, udanganyifu na matumizi mabaya ya taarifa binafsi.

Ripoti ya WHO kuhusu tabia za kiafya za watoto wa umri wa kwenda shule iliyotolewa mwaka 2024 pia ilionyesha kuwa matumizi yenye matatizo ya mitandao ya kijamii yanaongezeka miongoni mwa vijana katika nchi nyingi za Ulaya na Asia ya Kati, jambo linalochochea wito wa kuwepo kwa sera kali za ulinzi wa watoto.

Mbali na Ufaransa, mataifa kadhaa yameanza kuweka masharti makali kuhusu umri wa watumiaji wa mitandao ya kijamii. Australia, kwa mfano, ilitangaza hatua za kuimarisha ukaguzi wa umri wa watumiaji, huku baadhi ya majimbo nchini Marekani yakipitisha sheria zinazohitaji idhini ya mzazi kwa watoto wanaotaka kufungua akaunti za mitandao ya kijamii.

Kwa sasa, macho ya nchi nyingi za Ulaya yanaelekezwa Ufaransa kuona namna sheria hiyo itakavyotekelezwa na iwapo itatoa matokeo yaliyokusudiwa katika kupunguza madhara ya matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *