NI suala la muda tu, Singida Black Stars  kumalizana na kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Jean Charles Ahoua ili kuwa sehemu ya kikosi chao kwa msimu ujao.

Kwa mara ya kwanza Ahoua kucheza Tanzania alisajiliwa na Simba msimu wa 2024-2025 akawa kinara wa ufungaji katika Ligi Kuu Bara akifunga mabao 16, pia akimaliza na asisti tisa, akaondoka Januari 2026 kwenda kujiunga na CR Belouizdad ya Algeria.

Chanzo cha ndani kutoka Singida Black Stars kilisema viongozi wapo hatua ya mwisho kukamilisha usajili wake na muda wowote anaweza akatangazwa kuwa sehemu ya kikosi hicho.

Ahoua ambaye alizaliwa Februari 10, 2002 (umri wa miaka 24) nchini Ivory Coast, hakucheza kwa muda mrefu katika klabu ya Belouizdad, akidumu kwa takribani miezi sita kabla ya Singida kuanza harakati za kumrudisha Tanzania.

Chanzo hicho kimesema: “Tunaandaa timu yenye ushindani wa hali ya juu, kwa maana safu ya ushambuliaji itakayozalisha mabao mengi, viungo wazuri pamoja na mabeki.”

Chanzo hicho kimeongeza: “Ndio maana tumemrejesha Jonathan Sowah na kuwasajili wengine, lengo ni kufanya vizuri kimataifa na ligi ya ndani pamoja na michuano mbalimbali ya msimu wa ligi unaoanza Agosti 14, 2026.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *