Dar es Salaam. Wilaya ya Temeke imetajwa kuongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya waraibu wa dawa za kulevya mkoani Dar es Salaam, huku watu 2,500 waliokuwa wakitumia heroini wakipata huduma ya tiba mbadala ya methadone.
Takwimu hizo zimetolewa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), ikieleza kuwa Temeke ndiyo wilaya yenye idadi kubwa zaidi ya watu walioathirika na uraibu wa dawa za kulevya, ikifuatiwa na Kinondoni, Ilala, Ubungo na Kigamboni.
Akizungumza wakati wa tamasha la kupinga dawa za kulevya lililofanyika katika Viwanja vya Mwembe Yanga, leo Alhamisi, Julai 23, 2026, Kamishna wa Divisheni ya Kinga, Tiba na Urejeshwaji, Dk Cassian Nyandindi amesema tatizo la dawa za kulevya linaendelea kuwa kubwa katika Mkoa wa Dar es Salaam.
“Temeke inaongoza kwa kuwa na watu wengi walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya. Watu 2,500 waliokuwa wakitumia heroini wanatumia huduma ya methadone, jambo linaloonyesha ukubwa wa tatizo katika wilaya hii,” amesema Dk Nyandindi.
Kamishna wa Kinga, Tiba na Urejeshwaji wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Dk Cassian Nyandindi akizungumza wakati wa tamasha la kupinga matumizi ya dawa za kulevya.
Amesema mbali na huduma ya methadone, watu 16,000 wenye changamoto za afya ya akili zinazohusishwa na matumizi ya dawa za kulevya wamepatiwa matibabu katika Wilaya ya Temeke tangu mwaka 2014.
Amesema kampeni na matamasha ya kupinga dawa za kulevya yana lengo la kuhamasisha jamii inatambua kuwa athari za dawa hizo haziishii kwa mtumiaji pekee bali hugusa familia na jamii kwa ujumla.
“Hakuna anayebaki salama mbele ya tatizo hili. Kama halitamuathiri mtumiaji moja kwa moja, litawagusa wanafamilia, majirani na jamii nzima. Ndiyo maana kila mmoja ana wajibu wa kushiriki mapambano dhidi ya dawa za kulevya,” amesema.
Amesema DCEA huendesha matamasha hayo kila mwaka katika kanda mbalimbali za nchi, zikiwamo Kanda ya Mashariki, Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini, Mtwara na Kanda ya Kusini, ikiwa ni sehemu ya kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya dawa hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amesema mazingira ya kijiografia ya wilaya hiyo yameifanya kuwa miongoni mwa maeneo yanayorahisisha usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya.
“Temeke ni eneo ambalo ni rahisi kutumika katika usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya kutokana na jiografia na mazingira yake. Ndiyo maana kuleta tamasha hili hapa ni fursa kwa wananchi kupata elimu na kushiriki katika mapambano dhidi ya tatizo hili,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda akizungumza wakati wa tamasha la kupinga matumizi ya dawa za kulevya lililofanyika katika viwanja vya Mwembe Yanga.
Amesema athari za matumizi ya dawa za kulevya ni za muda mrefu na mara nyingi waathirika hukabiliwa na changamoto kubwa za kiafya na kijamii ambazo si rahisi kuziondoa.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya vita dhidi ya dawa za kulevya yanategemea kukata mnyororo wa usambazaji sambamba na kupunguza idadi ya watumiaji.
“Kukata mtandao wa usambazaji si rahisi kwa sababu una hatua nyingi kuanzia uzalishaji, usafirishaji hadi kuhifadhi. Lakini tukifanikiwa kupunguza watumiaji, soko la dawa hizo litapungua na biashara hiyo itakosa nguvu,” amesema Mapunda.