
Raia wawili wa Ghana wamewasilisha ombi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wakiitaka kufungua uchunguzi wa awali kuhusu vitendo vya ukatili vinavyowalenga wageni nchini Afrika Kusini, wakisema kwamba muundo, ukubwa na kukaririwa mashambulizi yanayowalenga wahamiaji vinaweza kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Ombi hilo limewasilishwa na msemaji wa zamani wa serikali ya Ghana kuhusu masuala ya usalama, Palgrave Boakye-Danquah, na mchambuzi wa kupambana na ugaidi na usalama Emmanuel Kotin.
Waliowasilisha ombi hiilo wanadai kuwa “kuna muundo mpana na wa kimfumo” wa mashambulizi dhidi ya wahamiaji, na wanaishutumu serikali ya Rais Cyril Ramaphosa kuwa imeshindwa kuzuia, kuchunguza na kuadhibu uhalifu unaofanyika huko Afrika Kusini ikiwa ni pamoja na mauaji, mashambulizi na uporaji.
Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari, waombaji wamesema: “Kwa miaka mingi, ndugu na dada zetu wa Kiafrika wameuawa, kupigwa, na kufukuzwa kutoka majumbani mwao nchini Afrika Kusini.”
Wahamiaji kadhaa wa Kiafrika wameripotiwa kuuawa, huku wengine wakishambuliwa na nyumba na biashara zao zimeporwa. Vurugu hizo pia zimewalazimisha makumi ya maelfu ya watu kukimbia nchi hiyo.
ICC, ambayo hufuatilia na kufungua mashtaka ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, haijatia majibu kwa maombi hayo.
Waandamanaji wa Kiafrika Kusini wanawatuhumu raia wa kigeni kuwa ndio wanaosababisha matatizo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ajira, uhalifu, na mashinikizo kwa huduma za umma, ingawa wahamiaji wanaunda takriban 5% ya idadi ya watu wa Afrika Kusini, ambayo inahesabiwa kuwa ni ndogo kwa viwango vya kimataifa.
Wizara ya Mahusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini imepinga ombi hilo ikisisitiza kwamba nchi hiyo ina mfumo wa kisheria wa kisasa unaotoa dhamana na mifumo ya kupambana na ubaguzi na kutovumiliana katika aina zake zote.
Afrika Kusini imekuwa katika wakati mgumu kufuatia wiki kadhaa za machafuko ya chuki dhidi ya wageni (xenophobic) ambayo wakati mwingine yamesababisha vifo vya watu.
Kampeni ya kupinga wahamiaji nchini Afrika Kusini tayari imewalazimisha maelfu ya raia wa kigeni kurejea makwao, ikiwa ni pamoja na raia wa Ghana, Malawi, Msumbiji na Nigeria.