#HABARI: Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imekataa ombi la mshtakiwa Tundu Lissu la kutaka maelezo ya maandishi ya shahidi wa Jamhuri Kamishna Msaidizi wa Polisi George Wilbert Bagyemu kupokelewa kama kielelezo katika kesi ya uhaini inayomkabili kwa kile kilichoelezwa ombi hilo limeletwa kinyume na utaratibu.

Hilo limejiri ikiwa ni siku ya pili ya kusikiliza ushahidi kwa shahidi wa Jamhuri ACP George Wilbert Bagyemu ambaye ni Naibu Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kuulizwa maswali ya dodoso na mshtakiwa Tundu Lissu.

Tundu Lissu ametoa ombi hilo baada ya kumuuliza shahidi kuhusu ushahidi alioutoa Mahakamani hapo na maelezo yake ya maandishi ya kama anakubali yapokelewe na Mahakama na kutumika kama kielelezo chake upande wa utetezi na shahidi akakubali.

Hata hivyo, upande wa Jamhuri umepinga suala hilo kwa maelezo kwamba mshtakiwa ameleta ombi hilo kinyume na utaratibu huku wakirejea hukumu zilizowahi kutolewa na Mahakama ya Rufani kuhusu suala kama hilo.

Mawakili wa upande wa Jamhuri wameiambia Mahakama kuwa suala la mshtakiwa kutaka kutumia maelezo ya shahidi kama kielelezo katika utetezi wake haikufuata utaratibu hivyo ombi lake halina msingi wa kisheria na kuiomba mahakama isipokee kielelezo hicho ingawa shahidi wao amekubali lakini Mahakama lazima ifuate sharia.

Akijibu hoja za upande wa Jamhuri Tundu Lissu amekubaliana na hoja za Mawakili wa Serikali, na kusema yupo tayari kurudi nyuma kuanza upya kwa kufuata utaratibu ambao mawakili wa Serikali na Mahakama ya Rufani imeeleza hata hivyo mawakili wa Serikali wakasema kwa kuwa Mshtakiwa amekubali alikosea ombi hilo liondolewe na suala la kuanza upya nalo haliruhusiwi kisheria.

Akitoa uamuzi baada ya kusikiliza pande zote mbili Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiana na majaji wengine wawili Jaji James Karayemana, Ferdinand Kiwonde, amesema Mahakama inalikataa ombi hilo la mshtakiwa Lissu la kupokea kielelezo hicho kwa kuwa hata mshtakiwa amekubaliana na pingamizi hilo.

Baada ya uamuzi huo, Lissu ameendelea na maswali ya dodoso kwa shahidi Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP Bakyemu amemhoji kuhusu maelezo aliyoyaandika ya kuwa alitoa maudhui yenye maneno ya uchochezi kwa umma kama ni uhaini au sio uhaini na shahidi amejibu maneno hayo ni uhaini.

Lissu ameuliza maneno yanayoitwa ya uhaini yaliyopo kwenye hati ya maelezo ya shahidi ya “wanasema kitu kimoja sahihi hapa, msimamo huu unaashiria kuasi, ni kweli, ni kweli kwa sababu tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, kwa hiyo tunakwenda kukinukisha sanasana, huu uchaguzi tutauvuruga kwa sababu tunakwenda kukinukisha vibaya sana” kama yapo kwenye hati ya mashtaka na ni uhaini na shahidi Afande George akajibu ni hayapo.

Ameuliza katika maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini kuna cheo cha kiongozi wa ngazi yoyote au jina la Mamlaka ya Serikali ya ngazi yoyote limetajwa, shahidi akajibu hakuna.

Lissu pia ameuliza kuwa ni nani aliyeamua kuwa jalada hilo liwe la uhaini shahidi amejibu yeye ndiye alifanya maamuzi ya jalada hilo kuwa la uhaini baada ya kuona kuna viashiria vya uhaini na hayakuwa maelekezo kutoka kwa Naibu Kamishna Wa Polisi (DCP) Ramadhani Ng’azi ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Polisi Makosa ya Mtandaoni wala Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya jinai (DCI) Ramadhani Kingai.

Lissu amehoji kuhusu maelezo yaliyotolewa na mwandishi wa Jambo TV aliyepewa jina la “p” mkutano wa ndani uliongozwa na Lissu ambao wao walikuwa wakirekodi na kurusha mubashara na mitandao ya kijamii ya Jambo Tv kwa nini mashtaka hayo yawe kwake kuwa yeye ndiye aliyechapisha taarifa zenye maneno ya uhaini mtandaoni na kwa nini “p” hajashtakiwa kwa uhaini ambapo akijibu shahidi George amesema jambo hilo si kweli kwa sababu kwa maelezo ya “p” Lissu wakati hayo yakiendelea aliwatoa waandishi nje.

Kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho Oktoba 8, 2025.

Katika kesi hiyo, Lissu anashtakiwa kwa kosa moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39 (2) cha sheria ya kanuni ya adhabu ambapo inadaiwa mnamo Aprili 3, 2025 maeneo ya Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam akiwa chini ya utii na raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitamka maneno yenye nia ya kuzuia uchaguzi wa 2025 kosa ambalo Lissu enapinga sio kweli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *