Moja ya jinai muhimu zaidi zilizofanywa na Marekani katika karne ya 21 ni kuikalia kwa mabavu Afghanistan kwa miaka 20 na uhalifu wake nchini humo.
Kufuatia mashambulio ya Septemba 11, 2001, Marekani ilianzisha operesheni kubwa ya kijeshi nchini Afghanistan, ikidai kuwa inapambana na ugaidi na kuwaangusha wanamgambo wa Taliban, hali iliyopelekea kukalia kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka 20 na kuwepo kwa vikosi vya Marekani na NATO. Uvamizi wa Marekani na kuikalia kwa mabavu Afghanistan sio tu kwamba umeshindwa kuleta utulivu na maendeleo nchini Afghanistan, bali pia ulikuwa na matokeo mabaya kwa watu wa nchi hiyo.
Katika miongo miwili ya uvamizi huo, raia walilengwa kwa mashambulio ya kibubusa, na kusababisha janga kubwa la kibinadamu. Kulingana na ripoti ya Chuo Kikuu cha Brown, kati ya watu 770,000 na 801,000 wameuawa katika vita vya baada ya Septemba 11, kati yao takriban 312,000 walikuwa raia. Nchini Afghanistan, zaidi ya watu 176,000 wakiwemo maelfu ya watoto na wanawake wamepoteza maisha.
Mauaji makubwa katika kipindi cha kukaliwa kwa mabavu Afghanistan
-Mlipuko wa Kunduz (2015): Mnamo Oktoba 3, 2015, ndege ya Marekani aina ya AC-130 ilishambulia kliniki ya Madaktari Wasio na Mipaka katika jiji la Kunduz. Shambulio hilo liliua wagonjwa wapatao 50 na wafanyakazi na kujeruhi makumi ya wengine. Shambulio hilo lilidumu kwa dakika 29 na jengo hilo lilipigwa mara 211. Shambulio hilo la anga lilitekelezwa licha ya Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka kutoa viunganishi GPS vya hospitali hiyo kwa maafisa wa jeshi na raia wa Marekani na Afghanistan kufikia Jumanne, Septemba 29.

Awali Jeshi la Anga la Marekani lilisema operesheni hiyo ilifanywa ili kuvisaidia vikosi vya Marekani katika eneo hilo. Jenerali John Campbell, ambaye wakati huo alikuwa kamanda wa vikosi vya Marekani nchini Afghanistan, baadaye alidai kuwa shambulio hilo lilitekelezwa kwa ombi la wanajeshi wa Afghanistan ambao walikuwa wakishambuliwa na Taliban. Alitaja shambulio hilo kuwa kosa na akasema hatuwezi kushambulia kwa makusudi kituo cha matibabu kinacholindwa.
-“Kurushwa Mama wa Mabomu yote” Nangarhar (2017): Mnamo Aprili 13, 2017, Marekani ilidondosha moja ya bomu lake la nguvu zaidi lisilo la nyuklia kwenye wilaya ya Achin mkoa wa Nangarhar. Bomu hilo lilisababisha uharibifu mkubwa, vifo vya watu wapatao 100, uchafuzi wa mazingira, na mlipuko wa magonjwa ya ngozi na mishipa ya fahamu kati ya wakaazi wa eneo hilo.
-Uvamizi wa usiku na operesheni maalumu: Vikosi maalumu vya Marekani na NATO vilishambulia mara kwa mara raia kimakosa katika uvamizi wa usiku kwenye makazi ya watu. Katika baadhi ya matukio, familia nzima iliuawa, na kumekuwa hakuna uwajibikaji. Mauaji haya si tu kwamba hayakuleta usalama nchini Afghanistan, bali pia yaliacha kumbukumbu chungu ya uvamizi na dhulma katika vichwa vya watu. Vita iliyoanza kwa jina la kupambana na ugaidi yenyewe ikawa chanzo cha ugaidi na mateso.
Kuwatesa wafungwa
Wakati wa uvamizi wa Afghanistan, kituo cha kijeshi cha kizuizini cha anga cha Bagram kilikuwa ishara ya ukiukwaji wa haki za binadamu na vikosi vya Marekani. Kikiwa kaskazini mwa Kabul, kituo hicho kiliwashikilia maelfu ya wafungwa wa Afghanistan, wengi wao wakishikiliwa bila kesi na kinyume cha sheria. Mateso hayo yalijumuisha kunyimwa usingizi, kupigwa, kuwekwa katika maeneo yenye kuumiza na vitisho vya ngono.

Mnamo 2002, wafungwa wawili wa Afghanistan, Habibullah na Delavar, walikufa kutokana na vipigo vikali vya vikosi vya Marekani. Ripoti za mashirika ya haki za binadamu zilionyesha kuwa wasaili wa Kimarekani walitumia mbinu ambazo zilifikia kuwatesa na kukiuka mkataba wa Geneva. Kambi ya kijeshi ya Bagram ilikuwa ikifanya kazi hadi 2014, na baada ya hapo ilikabidhiwa kwa serikali ya wakati huo ya Afghanistan. Hata hivyo, kumbukumbu chungu za mateso na unyanyasaji wa kibinadamu huko bado inabakia katika kumbukumbu za watu wa Afghanistan.
Uharibifu wa miundombinu na mgogoro wa kibinadamu
Kukaliwa kwa mabavu Afghanistan kulipelekea kuharibiwa miundombinu ya afya, elimu na huduma za umma nchini humo. Viwango vya uhaba wa chakula vilipanda kutoka 62% hadi 92%. Mamilioni ya watu walikimbia makazi yao, na Afghanistan ikawa moja ya nchi masikini zaidi ulimwenguni. Umaskini pia uliongezeka kutoka 80% kabla ya vita hadi 92% baadaye, na utapiamlo miongoni mwa watoto wa chini ya miaka 5 uliongezeka kutoka 9% hadi 50%.
Mbali na mateso ya kimwili, athari za kisaikolojia za vita dhidi ya watu wa Afghanistan zilikuwa nyingi. Manusura wa mashambulizi hayo, hasa watoto, walipatwa na matatizo ya kiakili, mfadhaiko, na wasiwasi wa kudumu. Uwepo wa kijeshi wa Marekani pia ulichangia kuenea kwa vurugu, rushwa, na kutoaminiana katika jamii.
Kiwango cha uharibifu
Ukaliaji mabavu Marekani dhidi ya Afghanistan sio tu kwamba imeshindwa kufikia malengo yake yaliyotajwa, lakini pia uliacha urithi wa uharibifu, umaskini, vifo na mgogoro wa kibinadamu. Uzoefu wa Afghanistan ulionyesha kuwa uingiliaji kati wa kijeshi wa kigeni, haswa kwa malengo ya kijiografia, sio tu kwamba, sio suluhu bali yenyewe ni chanzo cha mzozo.