Upinzani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati umetangaza kuwa utasusia uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Disemba ambapo Rais Faustin-Archange Touadera atawania tena urais kwa muhula wa tatu.

Viongozi wa jukwaa la upinzani, BRDC, wamesema hawana imani na maandalizi ya uchaguzi huo.

Wapinzani hao wamesisitiza kuwa wanapinga uwezekano wa Touadera kugombea muhula mwingine wa tatu, ambao ni matokeo ya kura ya maoni kuhusu katika mpya iliyopitishwa mwaka 2023 ambayo iliondoa ukomo wa mihula ya urais.

Uchaguzi wa urais, ubunge, na serikali za mitaa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati unatarajiwa kufanyika Disemba 28.

Rais Touadera alitangaza rasmi nia yake ya kugombea tena urasi wiki iliyopita kabla ya siku ya mwisho ya kujiandikisha kwa ajili ya kinyang’anyiro hicho ambayo ni Oktoba 11.

‘‘BRDC haitobadilisha uamuzi wake wa kususia uchaguzi wa Disemba. Hatutoshiriki,” ameeleza mratibu wake Crespin Mboli Goumba, baada ya wito kutolewa tena wa kufanya mazungumzo na Touadera.

Awali mwaka huu kiongozi huyo alitangaza kuwa yuko tayari kufanya  mazungumzo na wapinzani, ambapo mkutano wa kwanza ulifanyika mapema mwezi Septemba, lakini haikutajwa baada ya hapo tarehe nyingine iliyopendekezwa na serikali tangu wakati huo kwa mazungumzo hayo kuendelea.

Rais Faustin Archange Touadera, aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2016 kuiongoza Jamhuri ya Afrika ya Kati na alichaguliwa tena kwa muhula wa pili katika uchaguzi uliofanyika mwaka wa 2020.

Licha ya kukosolewa, Rais Touadera anasifiwa kwa kuboresha  hali ya usalama nchini humo baada ya miaka mingi ya mizozo na machafuko…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *