Wakati zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi wa Bunge la Iraq lingali linaendelea, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewapongeza wananchi wa nchi hiyo kwa ushiriki wao katika uchaguzi huo na kuipongeza pia Tume Huru ya Uchaguzi (IHEC) kwa kuendelesha zoezi hilo kwa ufanisi.

“Katibu Mkuu anakaribisha kuendeshwa uchaguzi kwa utulivu na kwa utaratibu na anaamini kuwa, wadau wa kisiasa watadumisha moyo wa amani na kuheshimu mchakato wa uchaguzi wakati matokeo yake yanaendelea kusubiriwa,” imeeleza taarifa ya Katibu Mkuu huyo wa UN iliyotolewa na msemaji wake, Stephane Dujarric.

Kwa mujibu wa Dujarric, Katibu Mkuu wa UN amesisitizia umuhimu wa “mchakato wa kuunda serikali kwa wakati na kwa amani” utakaoakisi matakwa ya watu wa Iraq na kukidhi matarajio yao ya kupata uthabiti na maendeleo.

Gutteres amethibitisha tena msimamo wa Umoja wa Mataifa wa kuendeleza uungaji mkono wake kwa Iraq katika kuimarisha mfanikio ya kidemokrasia iliyopata nchi hiyo na kujenga “mustakabali wa amani na fanaka.”

Aidha, ametoa shukrani kwa kazi ya Ujumbe wa Usaidizi wa Umoja wa Mataifa Nchini Iraq (UNAMI), ambao jukumu lake la kutoa usaidizi katika uchaguzi wa nchi hiyo linakaribia kumalizika baada ya kuhudumu kwa zaidi ya miongo miwili.

Kwa mujibu wa IHEC, zaidi ya Wairaqi milioni 12, wakiwemo wafanyakazi wa vyombo vya usalama na watu waliopoteza makazi yao, walipiga kura zao katika uchaguzi wa bunge uliofanyika siku ya Jumatatu, ikimaanisha kuwa zaidi ya 55% ya watu waliotimiza masharti walijitokeza katika upigaji kura. Matokeo yanatarajiwa kutangazwa ndani ya saa 24 zijazo.

Waziri Mkuu Mohammed Shia al-Sudani amesifu uchaguzi huo na kuuelezea kama “hatua ya kuajabiwa kuelekea kwenye uthabiti na maendeleo makubwa zaidi”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *