
Duru za serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimetangaza kuwa, waasi wa M23, wakisaidiwa na jeshi la Rwanda wanaendelea kusonga mbele kuelekea eneo la Kivu Kusini.
Siku ya Jumamosi, waasi hao waliudhibiti mji wa kimkakati wa Luvungi, karibu na mpaka na Burundi, pamoja na vijiji kadhaa vinavyouzunguka.
Maelfu ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao huku mapigano yakizidi kupamba moto.
Msemaji wa Jeshi la Kongo DR amevieleza vyombo vya habari kuwa wanajeshi wa serikali wameondoka Luvungi ili kuepusha kutokea uharibifu mkubwa na kuwalinda raia.
Katika taarifa, jeshi limesema, makombora yaliyofyatuliwa kutokea ndani ya Rwanda yameshambulia jamii kadhaa katika uwanda wa Ruzizi, na kuua raia na kuharibu skuli, vituo vya afya na nyumba.
Vyanzo huru vimesema, waasi sasa wanasonga mbele kuelekea mji wa Uvira.
Hayo yanajiri siku chache tu tangu marais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda waliposaini makubaliano ya amani mjini Washington, Marekani mbele ya rais wa nchi hiyo Donald Trump, yaliyoelezewa na ikulu ya nchi hiyo kuwa ni ya “kihistoria”.
Marais Félix Tshisekedi wa DRC na Paul Kagame wa Rwanda walisafiri hadi mji mkuu huo wa Marekani kwa ajili ya utiaji saini huo, ambapo waliungana na viongozi kutoka mataifa mengine kadhaa ya Afrika.
Makubaliano hayo yanaifungulia njia serikali ya Marekani na makampuni ya nchi hiyo kuchota madini adimu na yenye umuhimu mkubwa yaliyoko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo…/