
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi amesema, Tehran imefikia hitimisho kwamba Marekani haiko tayari kwa mazungumzo ya manufaa kwa pande mbili, ya usawa na yanayofanyika kwa msingi wa kuheshimiana.
Araghchi amesisitiza kwa kusema: “mazungumzo ni tofauti na utoaji maagizo. Wao wnanataka kutoa maagizo, na mimi si mtu wa kusikiliza maagizo ya watu wengine”.
Huku akiashiria kwamba, hakuna historia ya kuripua kituo cha nyuklia cha shughuli za amani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefafanua kwa kusema: “kwa hivyo, hakuna itifaki au maagizo ya kuvikagua vituo kama hivyo”.
Katika mahojiano na Shirika la Habari la Kyodo la Japan, Araghchi amebainisha: “kwa bahati mbaya, baada ya makubaliano huko Cairo, nchi tatu za Ulaya na Marekani zilifuatilia kurejesha utaratibu wa ‘snapback’ katika Baraza la Usalama, ambao ulikuwa kinyume cha sheria na hatudhani kama wana haki ya kurejesha tena utaratibu huu.”
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza: “tumefikia hitimisho kwamba Wamarekani hawako tayari kwa mazungumzo yenye manufaa kwa pande zote, yanayofanyika kwa usawa na kuheshimiana baina ya pande mbili. Mara tu tutapofikia hitimisho kwamba wako tayari kwa mazungumzo kama hayo, tunaweza kuanza tena mazungumzo. Jambo la msingi ni kwamba mazungumzo ni tofauti na utoaji maagizo. Bado hatujashawishika kwamba wako tayari kwa mazungumzo ya dhati na ya kweli; wanataka kutoa maagizo, na mimi si mtu wa kusikiliza maagizo ya wengine”.
Halikadhalika, Araghchi amesema: “kwa ajili ya siku zijazo, Iran imeazimia kikamilifu kuendelea na mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani. Tungali tumeazimia na tunayo teknolojia”…/