
Ripoti mpya imebainisha kuwa angalau Wapalestina 110 wamepoteza maisha ndani ya magereza ya utawala haramu wa Israel tangu Itamar Ben-Gvir, kinara mwenye misimamo mikali wa chama cha ‘Nguvu ya Mayahudi’ , ateuliwe kuwa waziri wa ‘usalama’ mnamo Desemba 2022.
Kwa mujibu wa huduma ya habari ya Israeli Walla, taarifa zilizopatikana kuhusu idadi ya wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa kwa jina la ‘wafungwa wa usalama’ wanaoishi chini ya usimamisi wa Ben-Gvir tangu alipochukua wadhifa huo mwezi Desemba 2022, zinaonyesha kwamba angalau 110 kati yao waliuawa kati ya Januari 2023 na Juni 2025.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa idadi hii inaonyesha ongezeko kubwa na inawakilisha rekodi isiyo ya kawaida ikilinganishwa na takwimu zilizopo kutoka kwa miongo iliyopita. Aidha, ripoti hiyo ilisema kuwa hali ya wafungwa wa Kipalestina imeharibika kwa kiasi kikubwa tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mwezi Oktoba 2023 na kuongezeka kwa kampeni ya kukamatwa kwa Wapalestina.
Ripoti hiyo ilionyesha pia hali ya kipekee ya mateso wanayokutana nayo wafungwa, ambapo mara nyingi wanasema kuwa wanateseka kutokana na njaa ya kimakusudi na udhaifu mkubwa wa lishe. Kwa mujibu wa ripoti, Wapalestina waliotekwa kinyume cha sheria na utawala wa Israel wamepata upungufu mkubwa wa uzito, na wanashikiliwa katika seli zilizozidiwa na watu, giza, na hali mbaya ya usafi.
Wale waliokaribu na Ben-Gvir wanadai kuwa waziri huyo mwenye misimamo mikali anajivunia kushadidisha hali ngumu kwa Wapalestina waliotekwa. Hali wanayoshikiliwa wafungwa wa Kipalestina inatia wasiwasi mkubwa. Zaidi ya hayo, wafungwa hawa wanaendelea kukutana na mateso, unyanyasaji, na dhuluma za kimfumo.
Mashirika ya haki za binadamu yanaripoti kuwa Israel inaendelea kuvunja haki na uhuru wa wafungwa kama ilivyowekwa kwenye Mkataba wa Geneva wa Nne na sheria za kimataifa. Kituo cha Utafiti wa Wafungwa wa Kipalestina kinadokeza kuwa karibu asilimia 60 ya Wapalestina waliotekwa kinyume cha sheria katika magereza ya Israel wanakabiliwa na magonjwa sugu. Kwa huzuni, idadi kubwa ya wao wamepoteza maisha wakiwa magerezani au muda mfupi baada ya kuachiliwa, kutokana na uzito wa hali zao za kiafya.