Mamlaka za Sudan katika jimbo la Kordofan Kusini zimethibitisha maafa makubwa: shambulio la ndege isiyo na rubani la waasi wa RSF lililotokea Alhamisi, Desemba 4, hadi sasa limeua watu 114 na kujeruhi 71. Miongoni mwa waliokufa wamo watoto 63 na idadi hiyo ingali inaongezeka.

Gavana wa Kordofan Kusini amesema baadhi ya majeruhi, wakiwemo watoto na raia , wako katika hali mahututi, lakini alieleza matumaini kuwa idadi ya vifo haitazidi kuongezeka kadri matibabu yanavyoendelea kutolewa.

Waziri Mkuu wa Sudan, Dkt. Kamil Idris, alifanya mawasiliano ya simu na familia za waliokufa na kujeruhiwa katika mji wa Kalogi, eneo la Gadir. Idris alilaani mashambulizi yaliyolenga shule ya awali na hospitali mjini Kalogi, akiyataja kama “kitendo cha kinyama na kishenzi.” Aliongeza kuwa tukio hilo ni “uhalifu kamili wa kivita,” na kwamba kundi la RSF limekidhi vigezo vyote vya kutambuliwa kama kundi la kigaidi kutokana na kulenga makusudi raia, wakiwemo watoto wa shule ya awali.

Serikali ya jimbo la Kordofan Kusini imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na mashirika ya haki za binadamu kuchukua msimamo thabiti kukomesha ukiukaji huu, kulitambua RSF kama “kundi la kigaidi,” na kuwawajibisha washirika wake kwa kile kilichoelezwa kama “makosa ya kibinadamu yasiyovumilika.”

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) pia limeshutumu shambulio hilo, likilitaja kama “ukiukaji wa kutisha wa haki za watoto.” Katika taarifa yake, UNICEF ilisema zaidi ya watoto 10 wenye umri kati ya miaka 5 na 7 wako miongoni mwa waathirika.

Kwa mujibu wa takwimu, kati ya majimbo 18 ya Sudan, RSF inadhibiti majimbo yote matano ya Darfur magharibi, isipokuwa baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Darfur Kaskazini ambayo bado yako chini ya udhibiti wa jeshi. Jeshi la Sudan linashikilia majimbo mengine 13 yaliyosalia katika kusini, kaskazini, mashariki na katikati, ikiwemo mji mkuu, Khartoum.

Tangu Aprili 2023, mapigano kati ya jeshi la Sudan na RSF yamesababisha vifo vya angalau watu 40,000 na kuwalazimisha watu milioni 12 kuyahama makazi yao.

Serikali ya Sudan imekuwa ikizilaumu baadhi ya nchi za kigeni, hususan Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kwa kuunga mkono kundi la waasi wa RSF, madai ambayo UAE imekanusha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *