Kufuatia kuchukizwa sana kwa walimwengu na utawala wa Kizayuni, hasa baada ya mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo huko Palestina, baraza la mawaziri la utawala huo limetenga bajeti ya takriban dola milioni 750 ili kuboresha taswira yake duniani.
Miaka miwili ya mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita vimewafanya walimwengu kuelewa kwa undani sura na utambulisho halisi wa utawala wa Kizayuni. Serikali za nchi mbalimbali duniani kote pia zimekataa kupanua uhusiano na utawala huo, na wakati huo huo, zimepiga kura ya kuipinga Israel katika majukwaa ya kimataifa. Nchi nyingi na maoni ya umma yanaiona Israel kama mkiukaji mkubwa wa haki za binadamu kutokana na mashambulizi na mauajii yake makubwa dhidi ya watu wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza. Huko Ulaya na Marekani, wimbi kubwa la ukosoaji limeibuka dhidi ya sera za Israel, na baadhi ya vyuo vikuu na mashirika ya kiraia yanaendelea kutoa wito wa kususiwa utawala huo wa kibaguzi kiutamaduni na kisayansi. Kwa hivyo, utawala wa Kizayuni wa Israel unakabiliwa na mgogoro mkubwa wa uhalali, kimataifa. Zaidi ya hayo ni kwamba, taswira mbaya ya utawala huo ghasibu imefifiza sura ya Israel kama kivutio cha watalii na uwekezaji.

Serikali ya Israel, ambayo inajua vyema kiwango kikubwa cha chuki na hasira ya kimataifa dhidi ya utawala huu na taswira yake mbaya sana duniani kote, inawekeza pakubwa katika mradi mpya wa kukarabati taswira hasi iliyopo na kuwasilisha simulizi yake mpya ili kuboresha hali hiyo. Katika suala hili, Waziri wa Fedha, Bezalel Smotrich na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Sa’ar wamekubaliana kutenga shekeli bilioni 2.35 (karibu dola milioni 750) kwenye bajeti ya 2026 ili kutekeleza kampeni kubwa za matangazo duniani kote. Baraza la mawaziri la Israel lilitangaza katika taarifa yake kwamba bajeti iliyotengwa itatumiwa katika kampeni za mitandao ya kijamii, ushirikiano na mashirika ya kiraia na kualika jumbe mbalimbali zikiwemo za vinara wa maoni ya umma, maafisa wateule, wahamasishaji na watu wenye ushawishi kutembelea maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel. Katika muktadha huo, hivi karibuni ujumbe wa wahamasishaji (influencers) kutoka Kenya ulipelekwa kutembelea maeneo mbalimbali katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina la Israel, suala ambalo limekosolewa sana na wadau wa mitandao ya kijamii na watetezi wa haki za binadamu.
Sehemu ya bajeti hiyo inatumika kwa ajili ya propaganda za kusafisha sura ya Israel barani Ulaya na Marekani. Baraza la mawaziri la Israel linahofia kwamba maandamano dhidi ya utawala huo yatapanuka zaidi kote barani Ulaya. Huko Marekani pia, Israel inawatumia wanaharakati wa mitandao ya kijamii kuboresha sura yake baada ya kuchafuliwa zaidi na mauaji yake ya kimbari huko Gaza. Watu wenye ushawishi (influencers) na wanaharakati mtandaoni wanawasilisha simulizi nzuri kuhusu Israel kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya kupate pesa nyingi. Ni muhimu kutambua kwamba, lengo kuu la matangazo hayo ni kuwasilisha taswira ya Israel kama dola la kisasa na kivutio cha watalii. Kwa maneno mengine ni kwamba, maafisa wa Kizayuni wanaamini kuwa iwapo utalii katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu utaimarishwa tena, taswira ya utawala huo pia itaboreka.
Sambamba na propaganda hizo kubwa, Israel inatekeleza ajenda ya kuchafua, kupotosha na kudharaulisha simulizi za mashirika ya kimataifa kuhusu mgogoro wa Gaza. Baadhi ya propaganda hizo zinafanya jitihada za moja kwa moja kuchafua na kupotosha ripoti za mashirika ya kimataifa kuhusu mgogoro wa binadamu huko Gaza. Kwa hivyo, mpango wa baraza la mawaziri la Israel, sambamba na kutaka kutoa taswira chanya kuhusu utawala huo ghasibu na katili, pia unalenga kuhoji na kuwafanya walimwengu wasiamini kwamba kuna mgogoro mkubwa wa binadamu huko Gaza.
Jambo la mwisho ni kuwa, mbinu hii inaonyesha kwamba Tel Aviv inataka kubadilisha mtazamo wa umma kupitia propaganda na mahusiano ya umma, badala ya kurekebisha tabia na mienendo yake katika nyanja za kisiasa na kijeshi. Hata hivyo, hata ndani ya Israel kwenyewe, kuna mtazamo kwamba mipango kama hiyo haiwezi kusaidia kukarabati taswira mbaya na chafu ya Israel, kwa sababu utawala huo unakabiliwa na viwango visivyo vya kawaida vya hasira na chuki ya watu duniani kote.