
Marekani imeitaka Israel ibebe jukumu la kuondoa vifusi vikubwa vilivyotapakaa kwenye kila pembe ya Ukanda wa Ghaza baada ya zaidi ya miaka miwili ya vita vya kinyama na mauaji ya kimbari iliyofanya dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo, pamoja na uharibifu mkubwa uliosababishwa na mashambulizi yake ya anga na matingatinga ya kivita. Hayo yameelezwa na toleo la Alkhamisi la gazeti la kizayuni la Yedioth Ahronoth.
Gazeti hilo limemnukuu afisa mmoja mwandamizi wa kisiasa na kuripoti kuwa, utawala wa kizayuni umekubali ombi hilo la Marekani “kwa sasa,” lakini utaanza kwa kuondoa vifusi katika eneo moja la majaribio huko Rafah.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Washington inatarajia kuwa, Israel hatimaye, itaondoa vifusi katika eneo lote la Ghaza, kazi ambayo inaweza kuchukua miaka kadhaa na kugharimu zaidi ya dola bilioni moja.
Yedioth Ahronoth limeongeza kuwa, kwa sasa wadau wa Kiarabu na wa kimataifa wamekataa kufadhili kifedha mpango wa kuondoa vifusi hivyo.
Likiashiria uharibifu mkubwa uliofanywa na utawala wa kizayuni katika vita vya miaka miwili, gazeti la The Wall Street Journal linalochapishwa nchini Marekani limeripoti wiki hii kuwa, eneo la Ghaza limefunikwa na karibu tani milioni 68 za vifusi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP, linakadiria kuwa vifusi hivyo vina uzito sawa na wa Majengo 186 ya Empire State.
Empire State Building ni jengo refu maarufu la ghorofa 102 lililoko jijini New York, Marekani.
Vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza mnamo Oktoba 2023, hadi sasa vimeshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 70,300 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 171,000.
Usitishaji mapigano ulioanza kutekelezwa Oktoba mwaka huu nao pia haujakomesha maafa ya mauaji, ambapo hadi sasa Wapalestina wasiopungua 386 wameuawa shahidi kutokana na mashambulio ya jeshi la Israel katika maeneo tofauti ya Ghaza…/