WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewataka wakandarasi kuweka kipaumbele utu wa wananchi na kuondoa kero kila wanapotekeleza miradi ya ujenzi nchini, akisema huo ndiyo mwelekeo wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza mkoani Ruvuma, Ulega alisema katika kila mradi wa ujenzi, mkandarasi anapaswa kwanza kutekeleza hatua zitakazoruhusu wananchi kuendelea na maisha yao kwa urahisi na kulinda utu wao badala ya kujikita katika kumaliza ujenzi wa barabara.
“Kama umepewa kazi ya ujenzi, fikiria unawezaje kurahisisha maisha ya watu. Kama unaweza kuweka kalavati kuzuia maji kuingia kwenye nyumba za wananchi, weka kwanza kalavati halafu endelea na ujenzi.
“Kama kuna sehemu ya barabara imekamilika na una taa za usiku, weka taa. Kama kuna kitu unaweza kufanya watu wasikae kwenye foleni kabla hujamaliza ujenzi, fanya kwanza. Barabara ni utu na lengo liwe wananchi, si kujenga barabara pekee,” alisema.
Ulega aliyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Kitahi–Amani Makoro–Ruanda hadi Bandari ya Ndumbi yenye kilometa 85 kwa kiwango cha lami, unaotekelezwa na Kampuni ya China Railway Seventh Group (CRSG).
Alisema alifanya ziara hiyo kutokana na maelekezo ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ambaye alionesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo licha ya serikali kumlipa mkandarasi.
Akiwa eneo la mradi, Ulega alimuelekeza mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha wananchi hawapati adha kwa changamoto zinazoweza kutatuliwa mapema.
Akizungumza kwa niaba ya mkandarasi, Ofisa Mwajiri wa CRSG, Themistocles Rugabela, alimwomba Ulega afikishe salamu za kuomba radhi kwa Waziri Mkuu kutokana na kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi kwa kasi na ubora unaotakiwa.
Ulega alimwagiza mkandarasi kujenga vivuko vya wananchi, kuongeza upana wa mitaro na urefu wa makalavati katika eneo la Amani Makoro pamoja na kufunga taa za barabarani kuanzia Kitahi hadi Amani Makoro ili kurahisisha shughuli za kiuchumi usiku na mchana.
“Rais Samia Suluhu Hassan anataka baada ya kazi kukamilika, wananchi wake waone furaha na tabasamu. Hakikisheni ujenzi wa barabara na madaraja unazingatia utu wa wananchi,” alisema.
Aidha, alimwelekeza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha maegesho ya malori yanajengwa katika hifadhi ya barabara eneo la Amani Makoro ili kuepusha uharibifu
wa miundombinu.
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Ruvuma, Salehe Mkwama alisema mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 60.4 na umegawanyika katika sehemu tatu.
Alisema sehemu ya kwanza ya kilometa tano kutoka Kitahi hadi Amani Makoro imekamilika huku sehemu ya pili ya kilometa 35 kutoka Amani Makoro hadi Ruanda ikiwa imefikia asilimia 41 ya utekelezaji.
Mkwama alisema sehemu hiyo ilitarajiwa kukamilika Desemba 2025 lakini imeshindwa kutokana na changamoto mbalimbali, ingawa serikali imeendelea kuzitatua ili mradi ukamilike Aprili 2026.
Aliongeza kuwa mradi huo una taa 880 zitakazofungwa katika maeneo ya makazi na madaraja makubwa kwa ajili
ya usalama wa wananchi.
