
Umoja wa Mataifa kupitia Kamishna wake Mkuu wa Haki za Binadamu umesema, hatua za miongo kadhaa za Israel za kuwatenga na kuwabagua Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi inaoukalia kwa mabavu zinazidi kuongezeka, na kwa sababu hiyo umetoa wito wa kuutaka utawala huo ukomeshe “mfumo wake wa ubaguzi wa rangi wa apathaidi”.
Katika ripoti mpya aliyotoa Jumatano kupitia ofisi yake, Volker Turk amesema, “ubaguzi wa kimfumo” unaofanywa dhidi ya Wapalestina katika maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa “umezorotesha vibaya sana” hali za maeneo hayo katika miaka ya hivi karibuni.
“Kuna ukabaji wa kimfumo wa haki za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi,” ameeleza mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika taarifa yake na akafafanua kwa kusema: “iwe ni katika upataji maji, skuli, kukimbilia hospitalini, kutembelea familia au marafiki, au kuvuna mizeituni – kila kipengele cha maisha ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi kinadhibitiwa na kuminywa na sheria, sera na taratibu za kibaguzi za Israel”.
Katika taarifa yake hiyo, Turk amekwenda mbali zaidi kwa kusema: “hii ni aina mbaya zaidi ya ubaguzi wa rangi na utengaji, ambayo inafanana na aina ya mfumo wa ubaguzi wa rangi wa apathaidi ambao tumewahi kuuona hapo kabla”.
Wataalamu kadhaa wa kujitegemea wenye mfungamano na Umoja wa Mataifa wamekuwa wakiielezea hali katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na utawala wa kizayuni wa Israel kuwa ni ya “ubaguzi wa rangi wa apathaidi” lakini hii ni mara ya kwanza kwa mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa kutumia msamiati huo.
Halikadhalika, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN ameitaka Israel “ibatilishe sheria, sera na hatua zote za utendaji zinazoendeleza ubaguzi wa kimfumo dhidi ya Wapalestina, unaofanywa kwa msingi wa rangi, dini au asili ya mbari”.
Hivi sasa kuna zaidi ya walowezi wa kizayuni 500,000 wanaoishi katika vitongoji haramu vilivyojengwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu tangu 1967 ambayo ni makazi ya Wapalestina wapatao milioni tatu.
Vitendo vya ukandamizaji na mauaji ya Wapalestina wa Ukingo Magharibi yameshtadi katika miaka ya karibuni, hususan tangu Israel ilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza Oktoba 2023.
Tangu wakati huo hadi sasa, wanajeshi na walowezi wa Israel wameshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 1,000 katika Ukingo wa Magharibi…/