
Kenya inatazamiwa kuanza msako wa kitaifa Januari 2026 dhidi ya taasisi za umma ambazo zimeshindwa kutekeleza sheria inayohitaji kuanzishwa kwa vituo vya kulelea watoto (“creche”) kwa wafanyikazi wa kike.
Agizo hili la utekelezaji linatoka kwa Wizara ya Afya, huku maafisa wakisisitiza kwamba hitaji la kisheria si la hiari na ni lazima litekelezwe ili kuwalinda akina mama wanaofanya kazi na watoto wao.
Japo linaonekana kuchelewa, wazazi wengi wamelipongeza kuwa litasaidia hasa akina mama walio na changa moto ya kukosa mtu wa kumuachia watoto wanapokwenda kazini.
‘‘Nakumbuka vijana wangu wote wawili niliwanyonyesha kikamilifu miezi sita ya kwanza,’’ anakumbuka Fridah Archie, mzazi nchini Kenya. ‘‘ nililazimika kukimbia nyumbani kila baada ya saa chache kuwanyonyesha, huku kazi inanisubiri. Ilikuwa ngumu sana. Ningekua na sehemu hapo kazini mtoto wangu anaweza kuangaliwa ingekuwa rahisi zaidi.’’ Fridah anaambia TRT Afrika.
Wengi wanachukulia sheria kwa wepesi
Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, sehemu nyingi za kazi za umma – ikiwa ni pamoja na taasisi za elimu na ofisi za utumishi wa umma – zimechelewa katika kutenga maeneo salama na ya kuaminika ya malezi ya watoto, licha ya mfumo uliopo wa kisheria unaowalazimisha waajiri kutoa msaada huo.
Utekelezaji duni umeripotiwa kuvuruga utendakazi na kuchangia mfadhaiko na usumbufu miongoni mwa akina mama wanaofanya kazi ambao wanatatizika kusawazisha majukumu ya malezi na kazi.
Katibu Mkuu wa wizara ya Afya ya Umma, Mary Muthoni, amesema taasisi nyingi zimeichukulia sheria kwa wepesi , na kuonya kwamba utekelezaji utaanza Januari ili kuonyesha kwamba sheria hiyo ina uzito kamili wa kikatiba.
“Wazo hilo sio sahihi. Sheria hii si ya hiari. Kuanzia Januari, tutaitekeleza kikamilifu ili kuwalinda akina mama wanaofanya kazi na watoto wao,” alisema Muthoni.
Vituo vya malezi vinasaidia kupunguza ‘utoro’
Takwimu kutoka tafiti mbali mbali zilizofanywa na Shirika la Wafanyakazi ILO, na shirika la Fedha IFC, zinaonyesha ukosefu wa malezi ya watoto yenye muundo huathiri kwa kiasi kikubwa ushiriki wa wanawake katika nguvu kazi na ustawi wao.
Wanawake hupewa mgao usio na uwiano wa malezi ya watoto, mara nyingi hutumia saa nyingi zaidi kwenye kazi ya matunzo isiyolipwa kuliko wanaume, jambo ambalo linapunguza uwezo wao wa kutafuta ajira ya kulipwa, elimu, na maendeleo ya kazi.
Tafiti hizi pia zinaonyesha kuwa upatikanaji wa vifaa vya kutunza watoto mahali pa kazi, kama vile vyumba vya kunyonyesha na vituo vya malezi, unahusishwa na viwango vya juu vya unyonyeshaji wa kipekee na uendelevu wa ajira kwa mama wachanga.
Kutokuwepo kwa huduma za malezi ya watoto kunaweza kusababisha utoro, kupungua kwa tija, na kupunguka kwa kazi huku akina mama wakitatiza malezi ya watoto wachanga na mahitaji ya kazi, na hivyo kuimarisha vizuizi vya kijinsia katika ajira.