Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amewaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma.
Rais Dkt. Samia amesema mabadiliko ya uongozi ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa kuboresha utendaji wa Serikali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi, na kwamba uteuzi wa viongozi hao umezingatia uwezo, uzoefu, uadilifu na rekodi nzuri waliyonayo katika utumishi wa umma.
Rais Dkt. Samia amesema uteuzi wa Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi katika nafasi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu (Kazi Maalum) umetokana na uzoefu wake mpana, ukomavu wa kiuongozi na uelewa wa kina wa masuala ya Taifa, akibainisha kuwa dhamana hiyo inalenga kuimarisha ushauri na majukumu ya kimkakati ya Serikali.
Halikadhalika, amewapongeza viongozi wote walioteuliwa na kuwasihi wakatimize majukumu yao kwa kuzingatia viapo vyao, na kuwataka kutekeleza kwa wakati ahadi zilizotolewa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
Akitoa maelekezo mahsusi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda, Rais Dkt. Samia amemtaka kusimamia maandalizi ya Mashindano ya AFCON 2027 ambayo Tanzania ni mwenyeji, sambamba na kukuza vipaji vya wanamichezo vijana na kutumia michezo kama chombo cha ajira na umoja wa kitaifa.
#StarTvUpdate
