Baadhi ya wanawake Jijini Dar es salaam wameiomba serikali kupunguza gharama za matibabu ya ugonjwa wa saratani hasa ya mlango wa kizazi inayoongoza nchini na kusababisha vifo vya wanawake zaidi ya elfu sita kwa mwaka wengi wao wakishindwa gharama za matibabu.
Wanawake hao wamepaza sauti juu ya maumivu ya mzigo wa gharama za matibabu ya saratani wakati wa zoezi la upimaji kwa hiari linaloendeshwa kwa siku mbili na asasi ya Shujaa kwa kushirikiana na Malkia.
Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya Shujaa Cancer Foundation Gloria Akida amesema wanawake wengi wanagundulika na saratani wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa hivyo asasi hiyo inaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha elimu zaidi inafika kwa jamii juu ya ugonjwa huo.
Daktari kutoka Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani Taasisi ya Ocean Road Kandali Samweli, amewaasa wanawake na mabinti walio kwenye rika la kujamiiana kupata chanjo ya ugonjwa huo lakini pia kuzitambua dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi na kuwahi kituo cha huduma za afya.
Januari ni mwezi ambao Tanzania huutumia kama mwezi maalum wa kujenga uelewa wa jamii kuhusu ugonjwa wa saratani ambao kwasasa unaongoza kwa kuondoa uhai wa watu wengi nchini ambapo mabinti wa umri kati ya miaka 9 hadi 14 wanaweza kupatiwa chanjo ya kuzuia maambukizi ya kirusi cha papilloma huku walio kwenye umri wa kujamiana wakishauriwa kupima mara kwa mara.
#StarTvUpdate
