Rais wa Syria Ahmed Al-sharaa ametangaza siku ya Jumapili, Januari 18, makubaliano na Wakurdi wa Syria, yanayotoa nafasi ya kusitisha mapigano na kuunganishwa kwa vikosi vyao katika taasisi za serkali na vikosi vya usalama na ulinzi, baada ya siku mbili wanajeshi wake kusonga mbele kwa kasi katika maeneo yanayoshikiliwa na Wakurdi kaskazini na kaskazini mashariki mwa nchi. Mkuu wa vikosi vya Wakurdi amesema amekubali makubaliano ya kusitisha mapigano.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Makubaliano hayo ni pigo kubwa kwa Wakurdi, ambao walikuwa na matumaini ya kuhifadhi utawala wao huru, ambao umekuwapo kwa zaidi ya muongo mmoja.

Hati ya pointi kumi na nne iliyochapishwa na ofisi ya rais inatoa nafasi ya kuunganishwa kwa vikosi vya Wakurdi (SDF) na vikosi vya usalama vya Wakurdi katika Wizara ya Ulinzi na Mambo ya Ndani.

Pia inaeleza kukabidhiwa mara moja kwa serikali majimbo yanayodhibitiwa na Wakurdi ya Deir Ezzor na Raqqa, yenye wakazi wengi wa Waarabu, pamoja na jukumu la Damascus kwa wafungwa wa kundi la Islamic State (ISIS) na familia zao wanaozuiliwa katika magereza na kambi zinazodhibitiwa na Wakurdi.

Ahmed Al-sharaa amewaambia waandishi wa habari kwamba amesaini makubaliano hayo kwa njia ya video na mkuu wa vikosi vya Wakurdi vya SDF, Mazloum Abdi, ambaye hakuweza kusafiri kwenda Damascus kutokana na hali ya hewa. Kulingana na rais, ambaye alifuta ziara iliyopangwa kwenda Berlin, maelezo ya makubaliano hayo yatakamilishwa wakati wa mazungumzo na Bw. Abdi siku ya Jumatatu.

“Ninapendekeza kusitisha mapigano kabisa,” rais wa Syria amebainisha mara tu baada ya mkutano na mjumbe wa Marekani kwa Syria, Tom Barrack, ambaye alikuwa amekutana na Bw. Abdi siku iliyopita huko Erbil, Iraq.

Hatua ya mabadiliko

Marekani, ambayo imewaunga mkono wapiganaji wa Kikurdi wa Syria kwa miaka mingi lakini sasa pia ni mshirika mkuu wa Damascus, imekaribisha makubaliano hayo, huku Tom Barrack akiyaita “hatua ya mabadiliko, huku wapinzani wa zamani wakichagua ushirikiano badala ya mgawanyiko.”

Kabla ya shambulio la jeshi la Syria, mazungumzo kati ya serikali kuu na Wakurdi yaliyolenga kuunganisha taasisi zao za kiraia na kijeshi serikalini, chini ya makubaliano yaliyofikiwa mwezi Machi 2025, yalisimama. Katika ishara dhahiri ya nia njema, siku ya Ijumaa, rais aliwapa kwa agizo Wakurdi haki za kitaifa ambazo hazijawahi kutokea, hasa kutambua lugha yao kama rasmi. Hatua hii ilionekana haitoshi na utawala huru wa Wakurdi kaskazini mwa Syria.

Rais wa Syria, ambaye alimpindua Bashar Al Assad zaidi ya mwaka mmoja uliopita, alibainisha siku ya Jumapili kuhusu umuhimu wa “uhuru wa Syria juu ya eneo lake lote.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *