
Mshauri mkuu wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ameonya kwamba shambulio la makombora la Juni mwaka jana kwenye Kituo cha Anga cha jeshi la Marekani cha Al-Udeid huko Qatar linapaswa kuwa ukumbusho kwa Rais Donald Trump kuhusu azma na uwezo wa Iran wa kujibu kitendo chochote cha uchokozi.
“Rais wa Marekani, ambaye mara kwa mara huzungumzia shambulio lisilo na taathira dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, angefanya vyema pia kutaja tukio la kuchomwa kambi ya Al-Udeid ya Marekani kwa makombora ya Iran,” Admirali Ali Shamkhani alisema jana katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Shamkhani, ambaye alijeruhiwa wakati makazi yake yalipolengwa kwa mashambulizi ya Israel kwenye Vita vya Siku 12 Juni mwaka jana ameongeza kuwa: “Uhakika huu utasaidia kuunda uelewa halisi wa azma na uwezo wa Iran wa kujibu uchokozi wowote.”
Ujumbe wake ulitolewa muda mfupi baada ya vyombo vya habari vya Marekani kuripoti kwamba baadhi ya wafanyakazi wa kambi ya kijeshi ya Marekani huko Al-Udeid walikuwa wameshauriwa kuondoka kambini kufikia Jumatano jioni kutokana na wasiwasi kwamba mvutano unaoongezeka kati ya Tehran na Washington unaweza kusababisha mapigano ya kijeshi.
Mwezi Juni mwaka jana Iran ilishambulia kambi ya Al-Udeid nchini Qatar kwa makombora, ambayo ndiyo kubwa zaidi ya jeshi la Marekani katika Asia Magharibi, baada ya Marekani kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran kuunga mkono uchokozi wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Mashambulizi hayo ya Marekani na Israel yaliua zaidi ya watu elfu moja, wakiwemo baadhi ya makamanda wa jeshi na wanasayansi wa nyuklia.