
Maafisa wa serikali na wakazi wa kaskazini magharibi mwa Nigeria wamesema kwamba maelfu ya watu wamekimbia makazi yao wiki hii baada ya kiongozi wa genge lenye silaha kuwaamuru waondoke kwenye maeneo hayo.
Maafisa wanasema kwamba tishio hilo limetolewa na Bello Turji anayeongoza mojawapo ya magenge yenye silaha yanawatisha wakazi wa maeneo ya kaskazini magharibi mwa Nigeria yenye idadi kubwa ya Waislamu, akiwaua na kuwateka nyara raia, wakulima, wanafunzi na madereva kwa ajili ya kupata fidia.
Wakazi wa jamii ya kaskazini magharibi ya Tidibale wanasema kwamba Turji anashuku kwamba taarifa za kijasusi zilizotumwa na jamii hiyo kwa askari usalama zimesababisha operesheni za kijeshi za hivi karibuni zilizopelekea kuuawa mmoja wa watu wake.
Mratibu wa Jimbo la Sokoto, Basharu Altine Guyawa, amesema kwamba Bello Turji alitembelea Tidibale siku tatu zilizopita na kuwaua watu watatu ili kutekeleza agizo lake la jamii kuondoka, na kwamba: “Aliwaambia ikiwa mtu yeyote atabaki atauawa. Alisema hatabakisha hai hata kuku.”
Msemaji wa polisi wa Sokoto amesema raia walikuwa wakikimbia jamii ya Tidibale kwa hofu ya kushambuliwa, na kwamba polisi zaidi wamepelekwa katika eneo hilo kuimarisha usalama.
Mohammed Ibrahim, katibu wa Kamati ya Usalama wa Jamii, amesema kwamba “zaidi ya watu 3,000 wamehamishwa, wakiwemo wale waliohifadhiwa katika shule za mji,” akieleza kwamba “kuna mgogoro wa binadamu na kwamba shughuli za kielimu zimesimama.”
Tidibale iko yapata kilomita 100 mashariki mwa mji mkuu wa Jimbo la Sokoto. Wanaharakati wa eneo hilo wanaonya kwamba vijiji kadhaa vimeachwa bila watu huku vurugu za magenge yenye silaha zikiongezeka kaskazini magharibi mwa Nigeria.