Katika matamshi yake mapya ya vitisho, Rais wa Marekani amezililenga nchi zinazofanya biashara na Iran.
Rais Donald Trump wa Marekani kwa mara nyingine tena amezitishia nchi zinazofanya biashara na Iran na kujaribu kuzikatisha tamaa kuhusu kufanya biashara na Iran. Amesema: Nchi yoyote inayofanya biashara na Iran italipa ushuru wa forodha wa asilimia 25 kwa shughuli ya kibiashara.
Trump kwa mara nyingine tena amewatishia washirika wa kibiashara wa Iran, lakini matamshi hayo badala ya kuwa ishara ya stratejia mpya, ni kielelezo cha sera iliyochakaa ambayo Washington imeijaribu mara nyingi katika miaka ya karibuni na imeshindwa na kufeli.
Tishio la kuzitoza ushuru wa asilimia 25 nchi zinazofanya biashara na Iran kwa hakika ni jaribio la kuibua tena mashinikizo ya kiwango cha juu lakini kwa sura mpya; mashinikizo ambayo mara hii si tu yanaelekezwa kwa Tehran pekee yake, bali pia kwa washirika wa kibiashara wa Iran. Mwenendo huu una maana kuwa Marekani inaendelea kufanya jitihada za kuzidisha adhabu za kushirikiana na Iran kwa kupanua wigo wa vitisho na kutia sumu anga ya kiuchumi na kisiasa dhidi ya Tehran.
Ni wazi kuwa, kwa kauli kama hizi, kivitendo, Trump anadhihirisha kwamba wenzo wake mkuu katika sera ya kigeni ni lugha ya mashinikizo na mabavu. Hii ni licha ya kwamba uzoefu unaonyesha kuwa kauli hizi zinatumiwa na vyombo vya habari na kipropaganda badala ya kutumika kiutendaji. Kutekelezwa vitisho kama hivi kunaiingiza Marekani katika migogoro mikubwa ya kisheria na kibiashara na nchi mbalimbali ambazo aghalabu zinategemea sana soko la Iran na haziko tayari kuvuruga uhusiano wao wa kiuchumi kwa maamuzi ya upande mmoja ya Washington. Kwa mtazamo huu, vitisho vya Trump ni vita vya kisaikolojia na jaribio la kuibua wasiwasi katika uga wa kimataifa badala ya kuwa sera ya kutekelezeka.
Katika mazingira kama haya, vitisho vipya vya Trump vinaakisi aina fulani ya kukwama kistatijia badala ya kuwa ishara ya nguvu ya Marekani. Ni kugonga mwamba kulikosabababishwa na Washington kushindwa kubadilli mienendo ya Iran. Kwa kukariri sera za huko nyuma, Trump ameonyesha wazi kwamba hana wenzo mpya wa mashinikizo; na hivyo analazimika kuwasilisha mifumo ile ile ya zamani kwa mtindo mpya. Hasa ikizingatiwa kuwa, vitisho hivyo vimetolewa katika hali ambayo Marekani yenyewe inasumbuliwa na changamoto nyingi za ndani za kiuchumi na kisiasa. Kupanda kwa gharama za maisha, athari mbaya za sera za ushuru na tofauti kubwa katika muundo wa utawala wa Marekani, yote haya yamewafanya wachambuzi wengi wione misimamo hii ya Trump kuwa ni jitihada zenye lengo la kupotosha fikra za waliowengi na kutunisha misuli nje ya Marekani. Ni wazi kuwa, Trump anajaribu kuficha udhaifu wa ndani na kujiarifisha kama mwanasiasa mwenye msijmamo imara.
Mkabala wa kauli zote hizi, msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni imara na uko wazi kikamilifu. Tehran imekuwa ikisisitiza kuwa vitisho na mashinikizo si tu kwamba hayataandaa mazingira ya kufanyika mazungumzo, bali yatazidisha hali ya kutoaminiana. Kwa kuzingatia uzoefu wa miaka iliyopita, Iran inatambua vyema kwamba sera ya mashinikizo haiwezi kuzaa matunda, lakini pia inauweka upande wa pili katika nafasi dhaifu. Viongozi wa Iran wametamka wazi mara kadhaa kwamba Jamhuri ya Kiislamu haitaki kuzidisha hali ya mvutano lakini pia haitasalimu amri mkabala ya vitisho vyovyote.
Kwa hakika, misimamo ya Iran imeonyesha kuwa Tehran ni mshirika mwenye busara, lakini haikubali kufanya mazungumzo chini ya mashinikizo. Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisistiza mara kwa mara kwamba Tehran iko tayari kuchunguza njia mbalimbali za ufumbuzi wa kisiaisa kwa sharti la kuwekwa kando anga ya vitisho na ya kulazimishana.

Katika hali kama hii, matamshi mapya ya Trump dhidi ya washirika wa Iran yanapaswa kuonekana katika muktadha wa mkwamo wa kimkakati wa sera za Marekani dhidi ya Tehran. Baada ya miaka mingi ya vikwazo, vitisho, na shinikizo dhidi ya Jamahuri ya Kiislamu, Washington bado haijaweza kufikia malengo yake. Kwa hivyo, vitishio dhidi ya nchi zinazoshirikiana kibiashara na Iran vinaonekana zaidi kama jaribio la kutunisha misulii kuliko sera halisi na inayoweza kutekelezwa. Mbinu hii inaonyesha kwamba sera ya mashinikizo ya juu zaidi imefeli na kushindwa.