Chanzo cha picha, EPA
Nchi saba, zikiwemo Saudi Arabia, Uturuki na Misri, zimesema zitajiunga na Baraza la Amani la Rais wa Marekani Donald Trump, kulingana na taarifa ya pamoja.
Nchi hizo zitajiunga na Israel, ambayo tayari ilithibitisha hadharani ushiriki wake mapema.
Jioni ya Jumatano, Trump alisema kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin pia amekubali kujiunga, lakini Putin alisema nchi yake bado inachunguza mwaliko huo.
Hapo awali, ilidhaniwa kuwa baraza hilo lililenga kusaidia kumaliza vita vya miaka miwili kati ya Israel na Hamas huko Gaza pamoja na kusimamia ujenzi upya.
Hata hivyo, rasimu ya katiba iliyopendekezwa haijalitaja eneo la Palestina, na inaonekana kubuniwa ili kuchukua nafasi ya baadhi ya majukumu ya Umoja wa Mataifa (UN).
Bado haijabainika ni nchi ngapi zimealikwa kujiunga na chombo kipya cha Trump, Canada na Uingereza ni miongoni mwa nchi zilizoalikwa, lakini bado hazijatoa majibu yao hadharani.
Hata hivyo, Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Albania, Armenia, Azerbaijan, Belarus, Hungary, Kazakhstan, Morocco na Vietnam tayari zimekubali kujiunga.
Siku ya Jumatano, Vatican pia ilithibitisha kuwa Papa Leo amepokea mwaliko. Akizungumza na waandishi wa habari siku hiyo, Katibu wa Serikali wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, alisema Papa atahitaji muda wa kutafakari kabla ya kuamua iwapo atashiriki.
Unaweza kusoma;