Bunge la Ulaya limesimamisha rasmi mchakato wa kuidhinisha makubaliano yake ya kibiashara na Marekani, kutokana na vitisho vya Rais Donald Trump vya kutoza ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa za EU zinazoenda Marekani, iwapo umoja huo hautaafiki azma ya Washington ya kuitwaa Greenland.

Uamuzi huo uliofikiwa jana Jumatano ndilo jibu kali zaidi la Umoja wa Ulaya hadi sasa dhidi ya US, kwa kile maafisa kadhaa wakuu walichokielezea wiki iliyopita kama usaliti.

Bernd Lange, Mkuu wa Kamati ya Biashara ya Bunge la Ulaya, amesema kwamba hadi pale “vitisho [kuhusu Greenland] vitakapokwisha, hakuna uwezekano wa kufikia maelewano” kuhusu kuidhinisha makubaliano na Marekani, ambayo yangewapa Wamarekani enzi mpya ya ushuru wa ‘asilimia sifuri’ kwa mauzo mengi ya nje ya bidhaa za viwandani.

Lange hata hivyo amebainisha kuwa, azma ya EU ya kununua nishati yenye thamani ya dola bilioni 750 kutoka Marekani haitaathiriwa na hatua hiyo, kwani ni tofauti na makubaliano ya ushuru.

Katika ishara ya kuendelea kuzorota uhusiano wa nchi za Ulaya na Marekani, Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen alirejea Brussels baada ya kuhutubia Bunge la Ulaya, badala ya kuelekea Davos kukutana na Trump. Amerudi kujiandaa kwa mkutano wa dharura mjini Brussels unaofanyika leo Alkhamisi, kujadili machaguo mbali mbali ya EU, iwapo Rais wa Marekani atatekeleza vitishio vyake vya ushuru dhidi ya nchi za Ulaya.

Hii ni katika hali ambayo, Waziri Mkuu wa Ubelgiji Bart De Wever amesema, ni lazima Ulaya imueleze wazi Trump kwamba hali ilipofikia hivi sasa “Haiwezi Tena Kuvumilika”.

Amesema, kurejesha uwezo wa kiushindani wa Ulaya lazima kiwe kipaumbele kisicho na shaka, lakini amesisitiza kwamba matamshi aliyotoa hivi karibuni Trump kuhusu Greenland na vitisho vya ushuru yametoa changamoto zaidi kwa EU.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *