Dar es Salaam. Muziki wa Bongofleva unaendelea kushuhudia kuibuka kwa vipaji vipya vyenye uwezo mkubwa, na miongoni mwao ni msanii anayetupiwa sana macho na wenzake, Yasirun Yasin Shaban, maarufu kama Yammi.
Msanii huyu alizaliwa Mei 20, 2002 mkoani Tanga, na kukulia Dar es Salaam, jiji ambalo limekuza ndoto yake na kuigeuza kuwa kweli na sasa ni kati ya waimbaji wanaofanya vizuri huku akiombwa sana kolabo.
Yammi kwao ni mtoto wa kwanza kwa mama yake mwenye watoto wawili, na mtoto wa tatu kwa baba yake, jambo lililomjenga katika mazingira ya malezi yenye upendo na mchanganyiko wa tamaduni.
Jina lake la kisanii ‘Yammi’ lina maana ya kitu kitamu na chenye ladha ya kusisimua, tafsiri inayojitokeza wazi wazi katika muziki wake mzuri uliojaa mvuto, hisia na upekee katika sikio la kila shabiki.
Yammi, mkali wa kibao cha Nitadumu Naye (2024), tangu akiwa mdogo alianza kuonyesha mapenzi makubwa kwenye muziki, hasa alipokuwa shule ya msingi.
Hivyo ndoto yake ya kuwa mwanamuziki ilianza mapema, na kuendelea kukua alipofika shule ya sekondari, ambapo alishiriki katika mashindano ya kuibua vipaji na kujijengea ujasiri wa kusimama mbele ya watu.
Licha ya kuwa na vipaji vingine kama upishi na uchoraji, Yammi aliamua kuuelekeza moyo wake wote kwenye muziki, akiamini kuwa ili kufanikisha ndoto ni lazima mtu ajitoe kikamilifu.
Sababu kubwa ya kujitosa katika sanaa hii na kujituma kwake kumetokana na kuupenda muziki wa Kihindi, ambao umekuwa na ushawishi mkubwa katika ladha yake ya kisanii, mitindo, sauti na uwasilishaji wake.
Ushawishi huu umempa sifa na mwelekeo wa kipekee, tofauti na wasanii wengi wa kizazi chake ambao wamejikita kuimba aina za muziki ambazo zimezoeleka kama Bongofleva, Afrobeats, Amapiano na kadhalika
Anasema mara yake ya kwanza kuingia studio lilikuwa tukio la kihistoria kwake, kwani lilimpa imani kuwa ndoto zake zinaweza kutimia endapo ataendea kuweka juhudi kikamilifu.
Kwa mara ya kwanza Yammi alipata nafasi ya kurekodi baada ya kushirikishwa na RJ The DJ (Romy Jons) katika wimbo, Sina (2022).
Mwaka 2022, ulikuwa mwanzo mpya katika safari ya Yammi ya kimuziki, hiyo ni baada video zake za kuimba na kuigiza nyimbo mbalimbali kupitia mtandao wa TikTok kuvuma sana.
Video hizo zilimkutanisha na mashabiki wengi zaidi, na punde tu umaarufu huo ukamfungulia milango ya fursa, ikiwemo kupokea simu kutoka kwa msanii mkubwa nchini, Nandy ambaye alikuwa akimvutia pia.
Kupokea simu kutoka kwa Nandy kulileta picha nyingine kwake, picha hii ilionyesha kuwa kuja kufanikiwa kimuziki si ndoto tu, bali ni maisha halisi anayoenda kuyaishi siku si nyingi.
Nandy alikuja kumsaini Yammi katika lebo yake, The African Princess, kisha akamtambulishwa kwa mashabiki kupitia Extended Playlist (EP), Three Hearts (2023) yenye nyimbo tatu ambazo vilipokelewa vizuri.
Uamuzi huo wa kujiunga na The African Princess umeendelea kumjengea misingi imara ya ukuaji wake katika tasnia, huku akijipambanua kama msanii mwenye nidhamu na shauku kufika mbali.
Chini ya lebo hiyo, Yammi aliwania tuzo za Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi kupitia wimbo wake, Namchukia (2023) ambao video yake hadi sasa imetazamwa YouTube mara milioni 22.
Katika kipengele hicho ndani ya TMA, Yammi alishindana na Xouh (Lalala), Appy (Watu Feki), Mocco Genius (Mi Nawe) na Chino Kidd (Gibela) aliyeibuka mshindi.
Baada ya mafanikio ya kimuziki akitambulika na wengi kama mwimbaji mahiri, Machi 2025, lebo ya The Africa Princess ilitangaza kusitisha mkataba wake na msanii huyo kwa makubaliano ya pande zote mbili.
Hivyo kwa sasa Yammi anaendelea kufanya muziki bila lebo lakini cha kufurahisha kutoka kwake ni jinsi wasanii wenzake mbalimbali wamekuwa wakimshirikisha, kitu kinachothibitisha kuwa ana kipaji kikubwa.
Ndani ya miaka hii miwili, Yammi ameshirikishwa na waimbaji kama Rayvanny (Usingizi), Abdukiba (You), Dully Sykes (Raha ya Tunda), Barnaba (Nibusu), Vanillah (Ok?), Kusah (Umekonda), Lava Lava (Aste Aste) na kadhalika
Kwa sasa linakuja suala la msanii yupi wa kike anafaa kwa kolabo, basi Yammi amekuwa akitupiwa macho na wengi, na hata nyimbo anazoshirikishwa zimekuwa zikifanya vizuri.
Hata hivyo, safari yake bado ni ndefu, lakini msingi aliouweka unaonyesha wazi kuwa kipaji, nidhamu na ijasiri wa kujitoa vinaweza kumfikisha msanii mbali zaidi ya alivyodhani.