Mke wa Rais wa Uturuki, Emine Erdogan, ameshiriki katika Mkutano wa Tano wa Wake na Waume wa Rais, ulioandaliwa na Mke wa Rais wa Ukraine, Olena Zelenska, jijini Kiev, ambapo alilihutubia kongamano hilo kwa njia ya video.
Mkutano huo, uliofanyika chini ya kaulimbiu “Elimu Inayobadilisha Ulimwengu,” uliwakutanisha wake na waume wa marais, wataalamu wa kimataifa na watunga sera kujadili jinsi elimu inavyoweza kujenga ustahimilivu, amani, na maendeleo ya kijamii.
Pia, uliwasilisha matokeo ya utafiti wa kimataifa uliofanyika katika nchi 14 (ikiwemo Uturuki), kuhusu: “Elimu kama Chombo cha Kujenga Ustahimilivu Binafsi, Mtaji wa Kijamii wa Kitaifa, na Utamaduni wa Amani.” Utafiti huo ulihusisha maoni ya wanafunzi, walimu na wazazi.
Katika hotuba yake, Emine Erdogan alielezea elimu kuwa silaha yenye nguvu zaidi ya kukabiliana na migogoro ya sasa duniani.
“Katika dunia inayopitia masaibu ya njaa, umasikini, vita, uhamiaji na mabadiliko ya tabianchi, nguvu pekee inayoweza kuinua tena ubinadamu ni elimu,” alisema, akiongeza kuwa ni kupitia mifumo ya elimu inayojikita kwenye maadili na utu, pamoja na upatikanaji wa elimu kwa wote, ndipo dunia yenye haki na usawa inaweza kujengwa.