Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imetaja hatua za Rais wa Urusi Vladimir Putin kuwa hatari na zisizokubalika, na ikasisitiza kwamba NATO inasimama imara kulinda eneo la muungano wao na usalama.

Kwa kujibu, Ujerumani imeimarisha jukumu la jeshi lake Bundeswehr katika kulinda upande wa mashariki wa NATO, na kutuma ndege nne za kivita kufuatilia anga ya Poland hadi mwisho wa mwaka.

Nchini Ufaransa, kaimu waziri wa mambo ya nje Jean-Noël Barrot, amesema Ufaransa itamwambia balozi wa Urusi kuwa haitatishika na kwamba lazima Urusi ikome kujaribu maamuzi ya NATO.

Barrot alitaja uvamizi huo kuwa mkakati wa makusudi wa Urusi kutishia na kuujaribu muungano huo wa NATO. Kama sehemu ya jibu lake, Ufaransa itatuma ndege tatu za kivita za Rafale, pamoja na maafisa wake kulinda anga ya Poland na mpaka wa mashariki wa NATO.

Umoja wa Ulaya wawaita mabalozi wa Urusi na Belarus

Umoja wa Ulaya umewaita mabalozi wa Urusi na Belarus katika mikutano tofauti kuhusu shambulizi hilo la Urusi .

Msemaji wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Anitta Hipper
Msemaji wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Anitta HipperPicha: EU//Christophe Licoppe

Msemaji wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Anitta Hipper, amesema leo kwamba wameweka wazi msimamo wao pamoja na taarifa 27 mpya za ukiukaji wa makusudi wa anga wa nchi mwanachama mpya na kwamba watasimama kwa mshikamano kamili na Poland.

Mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine yasitishwa kwa muda

Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, amesema njia za mawasiliano ya amani kati ya Urusi na Ukraine bado ziko wazi na zinafanya kazi.

Peskov amesema wawakilishi wao katika mazungumzo hayo wana fursa ya kuwasiliana kupitia njia hizo, lakini kwasasa, huenda ni sahihi zaidi kusema yamesitishwa kwa muda.

Moscow imeghadhabishwa na mapendekezo ya nchi za Ulaya na Uingereza kutoa dhamana ya usalama kwa Ukraine ambayo inaweza kuhusisha kupeleka wanajeshi wa NATO nchini Ukraine baada ya makubaliano yoyote ya amani na kusema haiwezi kukubali hatua hiyo.

Peskov amesema kusitishwa kwa mazungumzo hayo kunasababishwa na mazungumzo kama hayo.

Ukraine yashambulia bandari ya Urusi

Shambulizi la droni za Ukraine katika bandari ya Primorsk kaskazini magharibi mwa Urusi, kwa mara ya kwanza limesababisha kusitishwa kwa shughuli za upakiaji kwenye kituo hicho kikubwa zaidi cha mafuta. Haya ni kwa mujibu wa vyanzo viwili vya sekta hiyo pamoja na jeshi la Ukraine.

Gavana wa eneo amethibitisha tukio hilo lakini hakuripoti kusitishwa kwa shughuli katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *