[ad_1]
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina ni chuki ya wazi dhidi ya thamani za uadilifu na ubinadamu duniani na vilevile ni shambulio dhidi ya mafundisho ya Mtume Muhammad SAW ambaye amesema: “Kumuua mtu asiye na hatia ni sawa na kuua binadamu wote.”
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, kikao cha ngazi za juu cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kwa ajili ya Maulidi na kuadhimisha mwaka wa 1,500 wa kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW), kilifanyika mjini New York, jana Jumatatu jioni.
Katika mkutano huu ambao ulifanyika chini ya ajenda ya “Utamaduni wa Amani na Ustahimilivu,” wazungumzaji wamezungumzia nyanja mbalimbali za shakhsia ya Mtume wa Uislamu na umuhimu wa kushikamana na miongozo mitakatifu ya Mtume na mafundisho sahihi ya Uislamu na kuitaja kuwa ni kigezo cha kuimarisha amani na kuishi pamoja kwa amani kati ya dini na makabila, kuunga mkono wanaodhulumiwa, kukabiliana na chuki za kikabila na kupambana na chuki dhidi ya Waislamu na Uislamu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi, amedokeza kwamba hatua ya kuadhimisha mwaka wa 1,500 wa kuzaliwa Mtume Mtukufu wa Uislamu (SAW) kwa usimamizi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ni ukumbusho wa mafundisho ya kibinaadamu yenye ikhlasi ya Mtume Muhammad SAW.
Amesisitiza kuwa, mafundisho ya Uislamu na ya Mtume Muhammad SAW yanaitaka jamii ya kimataifa kutazama kwa undani zaidi maadili ya kudumu ambayo yanadhihirika katika maisha yenye matukufu mengi ya Mtume Muhammad SAW. Ni maadili yanayovuka mipaka na dini na yanahimiza ushirikiano wa kina wa kitamaduni na kielimu, pamoja na ushirikiano wa kibinadamu ambao huimarisha kuheshimiana na kuelewana. Ni maadili yale yale ambayo yanahitajika mno leo ili kuunda uhusiano wa kirafiki zaidi kati ya mataifa na watu kwenye ulimwengu wetu huu uliojaa msukosuko.
[ad_2]
BONYEZA HAPA KUSOMA HABARI KAMILI