Akizungumza Jumatatu mwanzoni mwa mkutano wa viongozi wa ulimwengu katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaolenga kuzifufua juhudi za kuundwa kwa mataifa mawili ya Israel na Palestina, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ametangaza kuwa nchi yake italitambua rasmi taifa huru la Palestina.
Tangazo hilo lilipokelewa kwa shangwe kutoka kwa zaidi ya viongozi 140 wanaohudhuria mkutano huo unaofanyika mjini New York, Marekani.
Macron: Ni muda wa kumaliza mashambulizi
Macron amesema lazima wafungue njia kwa ajili ya amani, na kufanya kila lililo ndani ya uwezo wao ili kusababisha uwezekano wa suluhisho la mataifa mawili, ambapo Israel na Palestina zitaishi pamoja kwa amani na usalama.
Amesisitiza kuwa umefika wakati sasa wa kuwakomboa mateka 48 wanaoshikiliwa na Hamas, muda wa kumaliza vita umefika, kumaliza mashambulizi dhidi ya Gaza, mauaji na kuzuia watu kuyakimbia makaazi yao.
Saudi Arabia imeupongeza uamuzi wa Rais Macron wa kulitambua dola la Palestina ikisema ni wa kihistoria. Akizungumza katika mkutano huo ulioitishwa na Ufaransa na Saudi Arabia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia, Faisal bin Farhan Al Saud ameyataka mataifa mengine kuchukua hatua kama hiyo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema taifa huru la Palestina ni “haki na sio zawadi.” Katika hotuba yake, Guterres ameonya kuwa hali ya Ukanda wa Gaza haiwezi kuvumilika na inazidi kuzorota kila saa, hivyo kuna haja ya kuchukua hatua za haraka.
Baerbock azungumzia mizozo ya kimataifa
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock ametoa wito wa kuanzishwa kwa taifa “huru na lenye uwezo” la Palestina. Amesema taifa kama hilo linapaswa kuishi pamoja na taifa la Israel kwa amani na usalama na mipaka inayotambulika na ushirikiano kamili wa kikanda.
Baerbock alizungumzia pia mizozo ya kimataifa ikiwemo njaa katika Ukanda wa Gaza ulioharibiwa kwa mashambulizi, vita vya Ukraine, unyanyasaji wa kingono nchini Sudan, ghasia za magenge ya uhalifu Haiti, na matamshi ya chuki yasiyozuiliwa mtandaoni.
Serikali ya Israel inapinga hatua ya Palestina kutambuliwa kama dola huru, ikisema kufanya hivyo ni kuipa zawadi Hamas.
Aidha, Rais wa Marekani Donald Trump anaamini kuwa hatua ya mataifa ya Magharibi kulitambuwa taifa la Palestina kunamaanisha kulizawadia vilivyo kundi la wanamgambo wa Hamas kutokana na shambulizi lake dhidi ya Israel. Kulingana na Israel, hatua kama hizo zitadhoofisha matarajio ya vita hivyo kumalizika kwa amani.
Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas ametoa wito wa kufanyika mazungumzo na Israel, ili kumaliza umwagaji damu na kuleta amani.
Marekani yakosolewa kwa kuunyima visa ujumbe wa Palestina
Akiuhutubia mkutano huo maalum wa kilele kwa njia ya video, baada ya Marekani kumnyima visa ya kuhudhuria, Abbas amelaani mauaji ya raia, uvamizi unaofanywa na Israel, pamoja na mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, 2023.
Hatua ya Marekani kumnyima visa Abbas pamoja na ujumbe wake kuhudhuria mkutano huo, imekosolewa na Guterres.
Viongozi wengine waliozungumza katika mkutano huo siku ya Jumatatu, ni Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, na Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney. Trump atauhutubia mkutano huo Jumanne, huku akitarajiwa kuzungumzia mada hiyo yenye utata.
(AFP, AP, DPA, Reuters)