
Wajumbe wa Israel wanatarajiwa kufika katika mji wa Sham el Sheikh, kwa majadiliano kuhusu kuachiwa mateka wa Israel wanaozuiliwa Gaza, kama sehemu ya mpango wenye vipengele 20 wa Rais Donald Trump wa kumaliza mzozo wa miaka miwili kwenye Ukanda huo wa Gaza.
Ujumbe wa Israel unajumuisha maafisa kutoka mashirika ya kijasusi Mossad na Shin Bet, Mshauri wa masuala ya sera za kigeni wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, Ophir Falk, pamoja na mratibu wa mateka Gal Hirsch. Mpatanishi mkuu wa Israel Ron Dermer, anatarajiwa kusafiri kuelekea Misri baadae wiki hii kushiriki pia mkutano huo.
Hamas kwa upande wake itaongozwa na kiongozi aliye uhamishoni Khalil Al-Hayya, ambaye ziara yake ya Misri ndio ya kwanza tangu aliponusuruika shambulizi la Israel mjini Doha mwezi uliopita. Yeye pamoja na wajumbe wenzake, wanalenga kutafuta majibu na njia za kutekeleza mpango wa kuwarejesha mateka wote walioko hai na waliokufa ili na wao, warejeshewe wafungwa wa kipalestina wanaozuiliwa Israel kwa muda mrefu pamoja na jeshi la Israel kuondoka Gaza.
Suala la kuwapokonya Hamas silaha ndilo gumu kufikiwa
Suala litakaloleta mvutano linasemekana kuwa masharti kutoka Israel, linalohusu mpango wa kuwapokonya Hamas silaha, jambo ambalo kundi hilo limesema haliwezi kutokea kamwe hadi pale Israel itakapoacha kuizingira Gaza, na kuuundwa rasmi dola la Kipalestina.
Hata hivyo waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ambaye nchi yake imekuwa ikitengwa katika siku za hivi karibuni kutokana na vita vyake vya Gaza vilivyodumu miaka miwili, amesema Dola la Palestina haliwezi kuundwa akikaidi baadhi ya mataifa ya Magharibi ambayo yameitambua Palestina kama dola huru ikiwemo Australia, Canada, Uingereza na Ufaransa.
Duru kutoka kwa afisa mmoja nchini Misri zinasema majadiliano yatakuwa magumu na makubaliano ya haraka hayawezi kupatikana mara moja.
Mpango wa Trump ni wa kutia moyo
Licha ya hayo bado kuna matumaini ya usitishaji wa vita hasa baada ya pande hizo kuukubali mpango wa Trump unaolenga kufanikisha hilo. Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi, amesema anamshukuru Trump kwa mpango huo baada ya miaka miwili ya vita, mauaji ya kimbari na uharibifu wa mali. Amesema pande hizo mbili zipo katika njia ya sawa ya kukomesha mateso kwa wapalestina.
Nae Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Johann Wadephul, amesema hatua zinazochukuliwa sasa za kujaribu kumaliza mgogoro huo zinatia moyo. Amesema kwa mara ya kwanza tangu vita hivyo kuanza Oktoba 7 mwaka 2023, hatua zinazochukuliwa sio tu za kusitisha vita lakini za kutafuta suluhu ya kudumu ya kisiasa ya mzozo huo wa Mashariki ya kati.